SERIKALI YAIOMBA ACBF KUJENGEA UWEZO WATAALAMU KWENYE MASUALA MTAMBUKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 7 February 2025

SERIKALI YAIOMBA ACBF KUJENGEA UWEZO WATAALAMU KWENYE MASUALA MTAMBUKA

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia), akiwa na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (Africa Capacity Building Foundation – ACBF), Bw. Mamadou Biteye, wakati walipokutana na Kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara ya Fedha, jijini Dodoma, ambapo walijadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na taasisi hiyo hasa katika maeneo ya vipaumbele ya kujenga uwezo wataalamu yanayolingana na Mpango Mkakati wa ACBF wa 2023–2027.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia), akimsikiliza Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (Africa Capacity Building Foundation – ACBF), Bw. Mamadou Biteye, wakati walipokutana na Kufanya mazungumzo katika ofisi za Wizara ya Fedha, jijini Dodoma, ambapo walijadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na taasisi hiyo hasa katika maeneo ya vipaumbele ya kujenga uwezo wataalamu yanayolingana na Mpango Mkakati wa ACBF wa 2023–2027.

Na Joseph Mahumi, Dodoma

SERIKALI imeiomba Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (Africa Capacity Building Foundation – ACBF) kuwajengea uwezo zaidi wataalamu nchini na kuweka kipaumbele kwenye masuala ya ufadhili katika Mabadiliko ya Tabianchi, Nishati safi, Kilimo Biashara, usalama wa Chakula, Biashara, Uwekezaji na Utawala wa kiuchumi na kijamii.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati alipokutana na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (Africa Capacity Building Foundation – ACBF), Bw. Mamadou Biteye, katika ofisi ya Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.

Dkt. Mwamba alisema kuwa, vipaumbele hivyo vinalenga kuleta mapinduzi katika kujenga uwezo nchini sambamba na masuala ya sayansi na teknolojia, ubunifu na kidigitali, uchumi wa buluu, na diplomasia ya kiuchumi, kwa kuwa vinawiana kwa ukaribu na Mpango Mkakati wa ACBF wa 2023–2027.

“Tunashukuru kwa fursa ya kushiriki katika mipango ijayo, hasa ile inayolingana na maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati wa ACBF wa 2023–2027, kwani maeneo hayo yanahusiana kwa karibu na vipaumbele vyetu vya kitaifa vya kujenga uwezo”

Aidha Dkt. Mwamba alisema kuwa Tanzania imekuwa mnufaika mkubwa wa taasisi hiyo tangu mwaka 1993 ambapo hadi sasa imefanikiwa kupata msaada wa takriban jumla ya milioni 9 zilizoenda katika taasisi mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar, Mtandao wa Kielektroniki wa Jamii wa Tanzania (TANZANET) na REPOA, ambazo zimeimarisha uwezo wetu kama taifa.

Aliongeza kuwa, katika kukabiliana na changamoto za karne ya 21, umuhimu wa kujenga uwezo hauwezi kuepukwa ili kukabiliana na changamoto hizo ipasavyo zikiwemo Utofauti wa Uchumi, Ukuaji wa Teknolojia, mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha taasisi zinakua imara imara sambamba na rasilimali watu wenye ujuzi, hivyo jukumu la ACBF linabaki kuwa la umuhimu mkubwa.

“Tunafarijika kuona kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nufaika wa mradi mpya wa kuongeza uwezo na kuleta Mabadiliko ya Kimuundo Afrika (Capacity Development for Africa’s Structural Transformation (CADAST) project), ambayo italeta mapinduzi katika kuimarisha usimamizi wa uchumi na fedha, na matumizi bora ya rasilimali za umma” aliongeza Dkt. Mwamba.

Naye kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Kujenga Uwezo Afrika (Africa Capacity Building Foundation – ACBF), Bw. Mamadou Biteye, alisema kuwa Miongoni mwa vitu walivyovibaini kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ni kwamba, kiwango cha kutumia fedha zinazotolewa na Mashirika ya kimataifa ni mdogo sana, ambapo kwa upande wa Benki ya Dunia kiwango ni asilimia 30 tu na asilimia 70 ya fedha zinazotolewa hazitumiki.

Amesema kuwa mpango wa Mafunzo kwa nchi za Afrika kuhusu uwezo wa usimamizi wa miradi utasaidia kwa kiwango kikubwa katika kutumia fedha zinazotolewa.

“Tutaendelea kuimarisha uwezo wa sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji kwenye sekta ya Nishati kwa kuboresha sheria ndani ya nchi za Afrika, lengo ni kuchochea maendeleo ya sekta hiyo itakayoleta matokeo chanya kwa wananchi kwa kuwa Afrika bado ipo nyuma kwenye sekta ya nishati ukilinganisha na maeneo mengine,” aliongeza Bw. Biteye.

No comments:

Post a Comment