WADAU WA MALEZI, MAKUZI WAKUTANA KUJADILI MICHORO NA MAKADIRIO YA VITUO VYA KULELEA WATOTO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 30 October 2024

WADAU WA MALEZI, MAKUZI WAKUTANA KUJADILI MICHORO NA MAKADIRIO YA VITUO VYA KULELEA WATOTO

Na Projestus Binamungu

OFISI ya Rais - TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la kuhudumia Watoto ulimwenguni UNICEF imewakutanisha Wadau wa Malezi na Makuzi nchini kwa ajili ya kujadili na kutoa maoni juu ya michoro na makadirio ya gharama za ujenzi wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana. 

 

Akifungua kikao kazi hicho kilichofanyika mkoani Morogoro Oktoba 29, 2024 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. Amon Mpanju amewataka washiriki kutilia mkazo wa maeneo ya ujenzi wa vituo hivyo kuwa yenye uhitaji na ambayo ni rahisi kufikika, ili vituo hivyo viwe na tija kwa jamii husika.

 

Ujenzi wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, ni utekelezaji wa agizo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipotembelea ujenzi wa Mji wa mtumba na kushauri kijengwe kituo maalum kwa ajili ya kulelea watoto wa watumishi wa serikali watakao kuwa wanafanya kazi mchana katika ofisi hizo.

 

Kama sehemu ya kutoa hamasa ya ujenzi wa vituo hivyo sehemu mbalimbali hapa nchini, Rais Dkt. Samia alitoa kiasi cha fedha cha shilingi Bilioni tatu, ili kisaidie kuanza utekelezaji wa agizo hilo , lakini ujenzi huo haujaanza mpaka sasa kutokana na ukosefu wa mwongozo maalum wa namna ya kujengwa kwa vituo hivyo.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi huduma za Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais -TAMISEMI Bi. Subisya Kabuje, kukamilika kwa michoro hiyo pamoja na makadirio ya gharama za ujenzi wa vituo hivyo kunatoa taswira mpya kwa wadau, na wawekezaji ambao wangetamani kujenga katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo sasa wataruhusiwa kujenga kwa kufuata mwongozo utakaotolewa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI baada ya mchakato wa kukusanya maoni na kufanya maboresho ya michoro na gharama za ujenzi unaoendelea sasa kuwa umekamilika.

 

Kwa upande wao UNICEF ambao ni washirika wakuu katika utekelezaji wa lengo hilo wamesema uzoefu wao katika nchi zenye vituo vya kulelea watoto mchana , vituo hivyo vimeonekana kuwa na matokeo chanya hasa katika kubaini vipaji vya watoto na kuvikuza tangu wakiwa wadogo.

 

Mwakilishi wa UNICEF katika mkutano huo Bw. Patrick Kodjia ambaye ni mtaalam wa lishe amenukuliwa akisema “Ujenzi wa vituo hivyo hapa nchini , si tu vinatoa mazingira ya ulinzi kwa mtoto, lakini vinawawezesha wanawake wengi kuwa na muda wa kutosha wa kushiriki kwenye shughuli zao za kiuchumi bila wasiwas juu ya usalama wa Watoto wao”

No comments:

Post a Comment