TANZANIA NA CUBA ZASISITIZA KUKUZA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 31 October 2024

TANZANIA NA CUBA ZASISITIZA KUKUZA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI


SERIKALI ya Tanzania na Cuba zimesisitiza kukuza ushirikiano wa kimkakati ili kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kihistoria na kindugu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili Baba wa Taifa Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania  na Hayati, Fidel Castor Ruz wa Cuba.

Msisitizo huo umetolewa wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 30 Oktoba 2024 katika Kikao cha Ngazi ya Wataalamu ambapo ujumbe wa Tanzania ulishiriki kikao hicho katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ulaya na Amerika, Bi. Naomi Mpemba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, ameeleza kuwa na imani na wajumbe wa mkutano huo na kwamba Tanzania ipo tayari kushirikiana kwa dhati na Cuba kwa ajili ya maendeleo endelevu na ustawi wa nchi hizo mbili.

Aidha, ameeleza kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni matokeo ya ziara ya Makamu wa Rias wa Jamhuri ya Cuba, Mhe. Salvador Valdés Mesa nchini mwezi Januari, 2024 ambapo alikubaliana masuala mbalimbali ya ushirikiano na mwenyeji wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango na kuelekeza kufanyika kwa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba.

‘’Mkutano huu ni ushahidi tosha wa nia thabiti waliyonayo viongozi wetu na sisi wataalamu katika kukuza ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kwa kuweka mfumo rasmi wa ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya utekelezaji na kujitathmini mara kwa mara’’ alieleza Bi. Mpemba.

Ushirikiano kati ya Tanzania na Cuba licha ya kuwa imara kisiasa na kidiplomasia, pia umekuwa ngao muhimu ya kufungua fursa mbalimbali katika sekta muhimu kama vile: afya, elimu, utalii, biashara, uwekezaji na utafiti. Kadhalika ushirikiano huu umerasimishwa kwa Mikataba na Hati za Makubaliano ya Ushirikiano zenye taratibu za kisheria zilizopelekea kupatikana kwa fursa za ufadhili wa masomo, teknolojia mpya, mafunzo ya udaktari na kushirikishana pamoja utaalamu katika maeneo tofauti.

Hata hivyo, ameleeza kuwa bado kuna fursa mbalimbali katika ushirikiano wa Tanzania na cuba zinazohitaji kuwekewa mikakati ya kuzikuza na kuziimarisha kwa kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano.

Naye Kiongozi wa Ujumbe wa Kikao cha Wataalam na Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Ushirikiano wa Uwili katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Cuba, Balozi Carlos Hernandez ameeleza kuwa na matumaini na kikao hicho kuwa cha mafanikio kwa ustawi wa pande zote mbili na kusisitiza umuhimu wa kufanyika majadiliano ya kina na ya mafanikio katika kuimarisha ushirikiano wa kimkakati.

‘’ Kwa kile kidogo tulicho nacho tupo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kujenga uwezo na kutoa ujuzi hususan katika masuala ya teknolojia kwa maendeleo na ustawi wa pande zote mbili’’ alisema Balozi Hernandez.

Kikao hiki pamoja na masuala mengine kimejadili kukuza ushirikiano katika maeneo ya kimkakati kati ya Tanzania na Cuba ikiwemo ushirikiano katika sekta ya afya, kilimo na uzalishaji wa chakula, elimu na masuala ya utamaduni na michezo. Aidha, kikao hicho cha watalaamu ni maandalizi ya Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Tanzania na Cuba utakaofanyika tarehe 4 Novemba, 2024 jijini Havana, Cuba.

Kikao cha Ngazi ya Wataalamu pia kimehudhuriwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humprey Polepole na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Yordenis Despaigne Vera.

Tanzania na Cuba zilianzisha ushirikiano wa kidiploamsia mwaka 1962 mara baada ya uhuru wa Tanzania na mwaka 1986 zilisaini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano ya kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika uchumi, sayansi na ushirikiano katika masuala ya kitaalamu.

No comments:

Post a Comment