WAZIRI MKUU ANADI SABABU 10 ZA KUWEKEZA TANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 27 September 2024

WAZIRI MKUU ANADI SABABU 10 ZA KUWEKEZA TANZANIA





WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa sababu 10 zinazoweza kumfaya mfanyabiashara yeyote kutoka Marekani avutiwe kuwekeza nchini.

Amezitaja sababu hizo kuwa ni mahusiano imara, sera thabiti za kiuchumi, mazingira ya amani na uthabiti, nafasi ya kijiografia ya nchi, uwepo wa masoko makubwa, uwepo wa nguvu kazi ya vijana na miundombinu ya kidijitali. Nyingine ni miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, uchumi mpana na utawala bora na mfumo wa kodi wa haki.

Akifungua jukwaa la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani lililofanyika jana jana (Septemba 26, 2024) katika makao makuu ya ofisi za CITI, jijini New York, Marekani, Waziri Mkuu aliwaeleza wafanyabiashara hao kwamba Tanzania ni mahali sahihi pa kuwekeza mitaji yao na pana mvuto ambao hakuna mwekezaji anaweza kuukwepa.

Akielezea kuhusu uimara wa mahusiano, Waziri Mkuu alisema uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili ambao umedumu kwa zaidi ya nusu karne, unathibitisha mazingira rafiki kwa uwekezaji.

Kuhusu sera thabiti za kiuchumi, Waziri Mkuu alisema kwa zaidi ya miongo miwili wastani wa ukuaji wa uchumi ulikuwa asilimia 7 na mfumuko wa bei wa chini ulikuwa wastani wa asilimia 3.8 hadi kufikia Desemba, 2023. “IMF inakadiria kuwa kwa kiwango hiki cha ukuaji, Tanzania itakuwa na uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2028.”

Kuhusu suala la amani, alisema mazingira ya biashara ya Tanzania ni ya kutabirika, ya uwazi na yenye ulinzi dhidi ya kutaifisha mali, huku wawekezaji wakiruhusiwa kurudisha faida zao baada ya kulipa kodi. “Tanzania iko kwenye eneo la kistratejia kutokana na nafasi yake ya kijiografia. Inapakana na nchi nane, jambo ambalo linatoa fursa bora za biashara na kuwa kitovu cha biashara cha kikanda,” alisisitiza.

Kwenye upatikanaji wa masoko makubwa, Waziri Mkuu alisema Tanzania inafikia soko la ndani lenye zaidi ya watu milioni 62, na zaidi ya watu milioni 500 kupitia jumuiya za kikanda kama vile SADC na EAC. Kuhusu nguvu kazi ya vijana, alisema Tanzania ina idadi kubwa ya vijana, ikitoa nguvu kazi ya kutosha inayoungwa mkono na uwekezaji katika elimu.

Akifafanua kuhusu miundombinu ya kidijitali, alisema Serikali inafanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kidijitali, jambo linaloifanya nchi kuvutia wawekezaji wa teknolojia. Kuhusu miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, Waziri Mkuu alisema Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), maboresho ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) na uwekezaji katika usafiri wa maji ni hatua zinazolenga kuimarisha biashara na usafirishaji nchini.

No comments:

Post a Comment