Na Mwandishi Maalumu
UBALOZI wa Tanzania umetia fora kwenye Tamasha la Mabalozi 2024 (Embassy Festival) nchini Uholanzi lililovutia watazamaji zaidi ya 50,000 wikiendi iliyopita mjini The Hague. Idadi hiyo ya wahudhuriaji nkatika Tamasha hilo ni pamoja na makumi ya wana Diaspora wa Tanzania waishio nchini humo pamoja na wawekezaji wakubwa kutoka Tanzania kama vile PetroBas NL.
“Tamasha hilo ni fursa ya kipekee kuonyesha utajiri wa utamaduni wa Tanzania, nasi nafasi hiyo hatukuipoteza hata kidogo,” Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi Mhe.Caroline Kitana Chipeta amesema.
Balozi Chipeta amesema fursa zilizojitokeza kwenya tamasha hilo ni kuanzia kukuza utalii na lugha ya Kiswahili hadi mchanganyiko wa mitindo ya zamani na ya kisasa, ambapo Tanzania iliibuka kuwa kivutia kikubwa.
Amesema Banda la Tanzania, likiwa na vyakula vya kuvutia na vifaa vya kitamaduni, lilikuwa kivutio kikubwa kiasi ya kwamba Mstahiki Meya wa The Hague, Jan Van Zanen, alifika na kulisifia huku akiongeza heshima zaidi ya Tanzania kwenye tukio hilo.
“Ujio wa Meya Zanen bandani kwetu kunaonyesha jinsi uwepo wa kitamaduni wa Tanzania ulivyothaminiwa sana huko The Hague”, amesema Balozi Chipeta
Katika tamasha hilo Tanzania ilifanya onyesho la mitindo na mbunifu wa Kitanzania la kuvutia sana, hasa kwa kuchanganya mavazi ya zamani na ya sasa ambako kulileta athari kubwa.
Balozi Chipets, ambaye yeye mwenyewe alishiriki akiwa kavalia vazi la mwanamke wa kimwambao la khanga na baibui na kushangiliwa sana, anasema, onesho hilo pia lilikuwa ni njia bora ya kuendeleza tamaduni za jadi huku zikifanywa ziwe za kisasa.
Banda la Tanzania pia lilikuwa kivutio cha pekee hasa kwa kucheza muziki pendwa wa Bongo Fleva ambapo kila aliyepita alifurahia, hasa hasa ilipopigwa ngoma ya Coma Cava ya Diamond Platinumz ambaye Septemba 30, 2024 atafanya onesho jijini Amtserdam.
No comments:
Post a Comment