NA MWANDISHI WETU,
ZANZIBAR
ASASI ya NMB Foundation
kwa kushirikiana na kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO) wamezindua mafunzo
endelevu kwa Wakulimwa wa Mwani Unguja na Pemba, ambapo Serikali ya Mapunduzi
ya Zanzibar (SMZ) imeipongeza na kuitaja asasi hiyo kama mbia wa karibu, wa
kimkakati na wa muda wote wa maendeleo Zanzibar.
Mafunzo hayo ya miezi
mitatu kwa wakulima zaidi ya 1,300 kutoka vikundi 72 vya wakulima,
yamefunguliwa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar
Said Shaaban, yakiwa ni zao la makubaliano ya ushirikiano yaliosainiwa Machi
mwaka huu kati ya NMB na Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO).
Akifungua mafunzo hayo,
Waziri Omar alizipongeza NMB Foundation na ZASCO kwa kuyaingiza makubaliano yao
katika vitendo kwa lengo la kuelimisha wakulima juu ya kilimo cha kisasa,
upatikanaji mikopo nafuu ya kilimo na kuwajengea uwezo wa elimu ya fedha kwa
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Machi mwaka huu
tulikutana Dar es Salaam kusaini makubaliano haya, tunaposimama hapa leo
tunaingia kwenye utekelezaji wa lile. Nawapongeza kwa sababu taasisi nyingi
zinasaini makubaliano, lakini ‘perfomance’ hakuna, NMB na ZASCO mmeenda mbali
zaidi katika hili.
“Mafunzo haya yanalenga
kujikita katika maeneo matatu ya elimu ya fedha, elimu ya kilimo na uzalishaji
na mwisho uwezeshaji wa kifedha kwa maana ya mikopo nafuu kwa wakulima wetu,
mambo yatakayowaongoza kulima kwa tija, kutunza fedha zitokanazo na mazao,
lakini kupata mitaji.
“Nawapongeza sana NMB
kwa jitihada zenu zisizokoma katika kuunga mkono Ajenda ya Serikali ya Zanzibar
ya Uchumi wa Buluu. Hakika sote ni mashahidi wa namna mnavyosaidiana nayo
katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za Wazanzibar.
“Kama kuna mbia wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambaye ni mbia wa karibu zaidi, mbia wa kimkakati,
lakini pia mbia ambaye wazungu wanamuita ‘of the all seasons,’ iwe mvua, kiangazi au masika, basi ni Benki
ya NMB, imekuwa ikishirikiana na Serikali katika mazingira yoyote yale,”
alisema Waziri huyo.
Kwa upande wake,
Mtendaji Mkuu wa ZASCO, Masoud Rashid Mohammed, alisema mafunzo hayo sio tu zao
la makubaliano ya taasisi zao katika kukuza uzalishaji wa mwani, bali ni
uthibitisho wa mlinganyo wa kimalengo waliyonayo, huku akizitaka taasisi zingine
za fedha kuiga mfano wa NMB.
“Mheshimiwa Waziri alisisitiza
vipaumbele vitatu vya awali kuwa ni Ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata Mwani
Pemba, alisisitiza hilo akisema ndio kipaumbele chake cha kwanza, cha pili na
cha tatu, lengo linalokaribia kutimia kwa sababu ujenzi unaendelea kwa kasi na
kufikia mwakani kitaanza kazi.
“Na katika kuhakikisha
kiwanda hakikosi malighafi za kuchakata, ndipo yalipozaliwa makubaliano yetu na
NMB na leo tuko hapa kuzindua mafunzo kwa wakulima 1,300 ili kuhakikisha
tunakuza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya kiwanda hiki, tukianza na vikundi
33 vya Pemba na 39 vya Unguja,” alibainisha Masoud.
Naye Meneja Mkuu wa NMB
Foundation, Nelson Karumuna, alimshukuru Waziri Omar Shaaban kwa kuwa sehemu ya
hafla ya awali ya kusainiwa makubaliano na hatimaye ufunguzi wa mafunzo hayo,
akisema ushiriki huo unaakisi dhamira ya SMZ katika kuwaletea maendeleo ya
Wazanzibar.
“Mafunzo haya yamelenga
kuwezesha wakulima kupata elimu ya fedha, uwezo wa kimtaji kwa maana ya mikopo
ya fedha na zana za kilimo. Unaweza kujiuliza kwanini tumechagua kuwapa na
elimu ya fedha wakulima hawa, jibu ni kuwa ndio muongozo wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
“Benki Kuu imesema wazi
kuwa elimu ya fedha ni nguzo muhimu sana katika kukuza uelewa wa kufanya
KilimoBiashara, sasa sisi tunajielekeza katika hiyo elimu ya fedha, NMB Benki
wao watawezesha katika suala zima la mikopo na ZASCO watafikisha elimu sahihi
ya kilimo.
“Sisi tunaamini kuwa
Programu hii ya mafunzo tunayoizindua leo, itaenda kuwa chachu ya kukuza
uzalishaji wa zao la Mwani hapa Zanzibar. Mafunzo yataanza hivi punde tuna omba
ushirikiano mkubwa tutapoenda huko kuwapa mafunzo, yushirikiano kutoka
Serikalini, kutoka ZASCO na Wakulima wenyewe,” alisema.
Awali, Mkuu wa Idara ya
KilimoBiashara wa NMB, Nsolo Mlozi, alisema taasisi yake inajisikia fahari
kufanikisha uanzishwaji wa mafunzo hayo kwa Wakulima wa Mwani ambao ni sehemu
ya mnyororo wa thamai wa kilimo unaohusisha kilimo chenyewe, ufugaji, uvuvi na
misitu.
“Sekta ya Kilimo ni
kati ya Sekta za Kimkakati na za kipaumberle kwa NMB, na ndio sababu
iliyotusukuna kushirikiana na NMB Foundation katika kuwanoa wakulima hawa, nasi
tunaahidi mikopo nafuu ya fedha na zana za kilimo ili kukuza uzajilishaji wa
zao hili hapa Zanzibar,” alisema.
No comments:
Post a Comment