Muonekano wa Daraja la Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 133 pamoja na barabara ya Kidatu - Ifakara yenye urefu wa kilomita 66.9 iliyokamilika kujengwa kwa kiwango cha lami ambalo leo tarehe 04 Agosti, 2024 imefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkoani Morogoro.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Serikali inakwenda kukamilisha ujenzi wa barabara zinazounganisha Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya Njombe na Ruvuma kwa kiwango cha lami.
Dkt. Samia ameeleza hayo leo Agosti 04, 2024 wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa upanuzi wa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Kilombero, Mkoani Morogoro.
“Mikoa ya Morogoro, Njombe na Ruvuma ni maeneo ambayo yanatoa chakula kingi sana na ni lazima tuhakikishe miundombinu inakuwa bora ili tuweze kutoa chakula kiende kwenye Soko, kwahiyo ni ahadi yetu na kama mnavyojua tukiahidi tunatenda”, amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia amewapongeza wananchi wa Wilaya ya Kilosa na Kilombero kwa kuwa wanufaika wa ukamilikaji wa Daraja la Ruaha Mkuu ambalo hivi sasa limeondoa changamoto zote zilizokuwepo hapo awali.
Dkt. Samia amewashukuru wafadhili kwa mchango wao wa kusaidia ujenzi wa barabara, daraja pamoja na Kituo cha kupozea Umeme ambao ni Shirika la Msaada la Uingereza (UKaid) na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU).
Aidha, Dkt. Samia amemuelekeza Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa kuhakikisha wanaendelea kufanya marekebisho au kujenga upya miundombinu ya barabara na madaraka katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua za El Nino kwa kuwa tayari fedha zipo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9) kwa kiwango cha lami na Daraja la Ruaha Mkuu (m 133) umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 157.15.
Bashungwa ameongeza kuwa ukamilikaji wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9) na Daraja la Ruaha Mkuu unaenda kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Kati kwa kuwa barabara hii inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Lindi kupitia Wilaya ya Kilosa, Kilombero, Ulanga na Malinyi zenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, ameeleza kuwa barabara ya Kidatu - Ifakara (km 66.9) na Daraja la Ruaha Mkuu imejengwa kwa kuzingatia viwango vya usanifu kwa mujibu wa mkataba ambapo ujenzi ulianza tarehe 02 Oktoba 2017 na kukamilika 30 Juni, 2024 kwa gharama ya Shilingi Billioni 157.15 ikijumuisha ujenzi, usimamizi na fidia ya mali zilizoathiriwa na mradi.
No comments:
Post a Comment