SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesaini mkataba wa kuongeza huduma kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Burundi Backbone System (BBS), kwa mkataba wa kibiashara wa Miaka Tano (5) wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 3.3/- sawa Shilingi za Kitanzania Bilioni 8.3/-.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) ameipongeza Burundi kwa kukubali kutumia huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB). Amesena hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kuboresha huduma za mawasiliano kwa wananchi.
"Kuunganisha Mikongo hii ya mawasiliano itakuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili. Kwa Tanzania, itawezesha upatikanaji wa soko jipya la huduma za mawasiliano nchini Burundi, na kuongeza fursa za biashara na uwekezaji. Kwa Burundi, itaboresha miundombinu ya mawasiliano nchini na kuimarisha uchumi wake kwa ujumla. Ninaamini kwa dhati ushirikiano huu utaimarisha uhusiano wa kindugu kati ya
nchi zetu mbili na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Afrika Mashariki kwa ujumla wake," alisema Mhe. Nnauye.
Aidha aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha dhamira thabiti ya kusimamia sekta ya mawasiliano nchini kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kukuza matumizi ya TEHAMA na huduma za kidijitali, na kufungua fursa kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC kutumia miundombinu yetu ya mawasiliano kama vile Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Eng. Peter Ulanga alibainisha kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umeleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali za uchumi, biashara, jamii na usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ameongeza kuwa TTCL imeendelea kusimamia na kuendesha miundombinu hii kwa weledi ili iweze kuendelea kuleta manufaa kwa Tanzania na pamoja na nchi jirani. NICTBB imeunganishwa kwenye mikongo ya baharini (submarine cables) kama vile SEACOM, EASSY na sasa tutajiunga na 2Africa, na kuifanya Tanzania kuwa kituo muhimu cha mawasiliano Kimataifa.
"Burundi Backbone System- BBS ni moja ya wateja wetu wa muda mrefu kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Tunajivunia uhusiano wetu nao tangu mwaka 2019, wakati tulipoingia Mkataba wa kwanza wa kuwapatia huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, kwa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Mkongo wa Burundi- Burundi Backbone System kupitia eneo la Kabanga mpakani mwa Tanzania na Burundi katika Wilaya ya Ngara, Mkoa wa Kagera na Manyovu kwa upande wa Kigoma," alisisitiza Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Eng. Ulanga.
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonesha dhamira thabiti ya kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ya kimkakati kama njia ya kufanikisha maendeleo ya nchi, hivyo malengo yake ni hadi kufikia 2025, Mkongo wa Taifa uwe umefikia Km 15,000 umeunganisha Mikoa na Wilaya zote.





No comments:
Post a Comment