SHIRIKA la CAMFED limeadhimisha miaka 25 ya utoaji huduma ya kusaidia wasichana wanaotoka katika mazingira magumu, ambao wanakutana na changamoto wakiwa shuleni na wengine kushindwa kutimiza ndoto zao, ikitokea wanakosa msaada. Wanufaika wa huduma hizo, ambao kwa sasa wengine ni viongozi, wafanyakazi, wafanyabiashara na wakulima wamekutaka Mjini Bagamoyo juzi kutoka katika nchi tano za Afrika, ikiwemo Zimbabwe, Zambia, Ghana, Malawi pamoja na Tanzania yenyewe kusherehekea mafanikio na kutathimini changamoto kwenye huduma zao.
Akizungumza na wanahabri nje ya mkutano huo, Mshauri Mkuu wa Shirika la CAMFED, Bi. Fiona Mazinga kutoka Zimbabwe, anasema maadhimisho hayo ya miaka 25 ya utoaji wa huduma kwa mabiti wanaotoka katika mazingira magumu yana maana kubwa kwao, hasa ukizingatia kuwa kwa sasa idadi ya wanufaika imeongezeka kiasi kikubwa ukilinganisha na hapo awali.
Anasema CAMFED ilianza kutoa huduma zake mwaka 1998 nchini Zimbabwe ikiwa na wasichana 400 tu, lakini hadi leo linatoa huduma zake kwenye nchi takribani 13 ulimwenguni, huku kwa Afrika ikiwa na nchi tano, zikiwa na idadi kubwa ya wanufaika. Alisema lengo la CAMFED ni kuhakikisha linawafikia wanufaika takribani 500,040 kwa nchi za Afrika ifikapo mwaka 2030.
Shirika la CAMFED Tanzania linafanya kazi kwa karibu na viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za vijiji, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba programu ambazo inazifanya zina fika mbali zaidi kwa jamii. "Ndio tunazianzisha sisi lakini tunapoishirikisha Serikali tuna amini hata kama CAMFED itaondoka eneo hilo basi jamii na Serikali nao wataendelea kuendesha program hizo, na kuwafikia watoto wengi zaidi.
Naye, Mkurugenzi wa Miradi na Ushirikiano wa Shirika la CAMFED Tanzania, Bi. Anna Sawaki, alibainisha kuwa kwa Tanzania, CAMFED inajihusisha na kusaidia mabinti wanaotoka kwenye mazingira magumu, ambao kama ikitokea wasiposaidiwa wanaweza wasifikie ndoto zao kielimu.
"Kwa hiyo tunawasaidia kwenye elimu kwa maana wao kupata mahitaji muhimu ili waweze kuendelea na masomo yao, lakini pia kwa kutambua elimu pekee inaweza isitoshe kumvusha mtoto wa kike kutoka kwenye utoto kwenda kwenye utu uzima, tumekuwa tukiwasaidia kwenye miradi ya mpito ikiwemo miradi ya stadi za maisha ili waweze kujitambua, pia tunawawezesha kwenye miradi ya ufundi, miradi ya biashara na miradi ya kilimo.
"CAMFED Tanzania tulianza mwaka 2006 na tulianzia mkoa wa Iringa tukiwa na mabinti 28 tu, lakini leo hii mwaka 2023 tumeweza kuifikia mikoa 10, Halmashauri 33, tukiwa na jumla ya wasichana wafadhiliwa takribani 57,000. Tunavyosema idadi ya wafadhiliwa imeongezeka tuna maanisha viongozi wapo ndani yake, kuanzia ngazi za vijiji hadi taifa, ndani yake tunawakulima wazuri sana, tunawafanyabiashara wazuri sana, tuna wasichana ambao wanajitolea kuwaongoza wenzao ili wasikwame kama wao walivyo kwama huko nyuma," anafafanua Mkurugenzi huyo wa Miradi na Ushirikiano wa CAMFED Tanzania, Bi. Sawaki.
Kwa upande wake, Bi. Dairis Christian, mmoja wa wafadhiliwa wa CAMFED kutoka Tanzania, ambaye kwa sasa ni Afisa Program Mwandamizi wa CAMFED Tanzania, anasema alipata kazi ndani ya taasisi hiyo mwaka 2012 baada ya kufadhiliwa hapo nyuma mwaka 2009, akiwa Chuo Kikuu baada ya kukwama kupata fedha za kuendelea na chuo.
"...kabla ya ufadhili wa masomo yangu nimetokea katika mazingira magumu na kujifunza mengi ilifikia mahali hadi nilitaka kuacha kabisa masomo yangu lakini program za CAMFED ndiyo iliniibua tena, tunaposherekea miaka 25 kwangu ina maana kubwa sana kwani bila CAMFED nisingeliweza kumaliza masomo yangu na kuwa mfanyakazi," anasema Bi. Dairis Christian.
Anaongeza kuwa akiwa na mtandao wa wafadhiliwa wa CAMFED amepata mafunzo mengi ambayo yameendelea kunijengea uwezo na kuwa kiongozi mzuri. "Naweza kusema sasa hivi mimi ni kiongozi maana ninao mabinti ambao nawaongoza na wanajifunza mengi kutoka kwangu nao wanaendelea kukabiliana na changamoto kadhaa katika masomo yao...nawashauri wasikate tamaa waendelee kupambana na watafikia tu ndoto zao," alisema Bi. Christian.

No comments:
Post a Comment