Na Elimu ya Afya kwa Umma
MGANGA Mkuu Mkoa wa Rukwa, Dkt. Ibrahim Isack ameipongeza Wizara ya Afya pamoja na wadau mbalimbali ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) pamoja na Save the Children kwa kuweka nguvu za pamoja kufanikisha Kampeni ya Chanjo ya Matone dhidi ya Polio.
Dkt. Isack ametoa pongezi hizo Mkoani Rukwa ikiwa Uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya Matone dhidi ya Polio kitaifa ulifanyika mkoani humo huku walengwa ilikuwa ni watoto walio na umri chini ya miaka 8 katika mikoa 6 ya Rukwa, Katavi, Kagera, Kigoma, Mbeya na Songwe.
"Kwa kweli Wizara ya Afya pamoja na wadau ikiwemo WHO, UNICEF na Save the Children wamekuwa na mchango mkubwa hususan suala uwezeshaji na uelimishaji kwa jamii,"
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa Catherine Mashalla amesema hamasa ya Elimu ya Afya kwa Umma imekuwa na mchango mkubwa kufikia jamii kupata chanjo ya Polio kwa watoto.
"Tunashukuru tumekuwa tukihamasisha jamii na Elimu ya Afya kwa Umma pamoja na Mpango wa Taifa wa Chanjo wametusaidia sana kupita sehemu mbalimbali na kutumia wimbo wa hamasa," amesema Mashalla.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Rukwa Ndenisia Ulomi amesema wadau wamesaidia katika ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ambapo jumla ya watoto 546, 026 wamepatiwa chanjo Mkoani Rukwa.
"Tumeshirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Wadau ambapo katika halmashauri ya Wilaya ya Kalambo lengo ilikuwa ni kuchanja watoto 80,486 waliofikiwa ni watoto 111,524 sawa na asilimia (138.56%), Nkasi DC lengo ni kuchanja watoto 109,514 na waliochanjwa ni watoto 145, 234 sawa na asilimia 132.62%, Sumbawanga DC lengo ni watoto 118,071 na waliochanjwa ni watoto 175,165 sawa na 148.36% na Sumbawanga MC lengo lilikuwa watoto 83,811 na waliochanjwa ni watoto 114,103 sawa na asilimia 136.14%"amesema.
Naye mwakilishi wa Save the Children George Sungwa amesema Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mkoa wa Rukwa pamoja na wadau wengine wamekuwa na mchango mkubwa katika Kampeni ya Polio.
Alex Mwembezi pamoja na Rusia Swaila ni miongoni mwa wakazi wa Mkoa wa Rukwa ambapo wamesema kutokana na hamasa ya Elimu ya Afya kwa Umma wamekuwa na uelewa juu ya chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio ikiwemo kuzuia kupooza.
Ikumbukwe kuwa Kampeni ya chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio ilianza Septemba 21-24, 2023 katika mikoa 6 ya Rukwa, Kagera, Katavi, Kigoma, Mbeya na Songwe na matarajio ya kuchanja ni zaidi ya watoto milioni tatu.
No comments:
Post a Comment