WANAFUNZI BORA SHAHADA YA SAYANSI YA HALI YA HEWA WAPEWA ZAWADI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 9 September 2023

WANAFUNZI BORA SHAHADA YA SAYANSI YA HALI YA HEWA WAPEWA ZAWADI






RAIS wa Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa Tanzania (TMS) ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa Barani Afrika, na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Buruhani Nyenzi amekabidhi zawadi kwa wanafunzi bora waliohitimu shahada ya kwanza ya hali ya hewa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 2019/ 2020, kwenye hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ubungo Plaza, Tarehe 08/09/2023. 

Katika hafla hiyo Bw. Innocent Junior alitunukiwa zawadi ya mwanafunzi bora wa jumla, ambapo Bi. Fatma Semgaya pamoja na Bw. Moh’d Msellem walitunikiwa zawadi ya kufanya vizuri zaidi katika somo la utafiti wa masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. 

Kabla ya kukabidhi zawadi hizo Dkt. Nyenzi aliwakumbusha kuwa TMS ilibuni njia ya utoaji zawadi kwa wahitimu vyuo vikuu waliofanya vizuri katika fani ya sayansi ya hali ya hewa ili kuleta hamasa na kuchagiza mwamko kwa wanafunzi kujiendeleza katika taaluma ya sayansi ya hali ya hewa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a aliwahimiza washiriki na hasa wanafunzi kujiwekea malengo makubwa ya kujijengea umahili na weledi, na kufanya kazi kwa bidii na uzalendo ili kuacha alama ya kile wanachokifanya katika taaluma zao. 

Aidha, Mwanafunzi bora kwa mwaka 2019/2020, Ndg. Innocent Junior alizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake na kumshukuru Dkt. Nyenzi, Mwenyekiti  wa chama cha TMS kwa kuwatunuku zawadi za kutambua umahili  walionesha katika masomo yao. 

Aidha aliendelea kumshukuru Dkt. Chang’a pamoja na wataalamu wengine wa hali ya hewa, ambapo mwaka 2016 walitembelea shule ya seondari ya Ilboru, iliyopo Arusha, yeye akiwa mwanafunzi, na kuwaelimisha na kuwahamasisha wanafunzi kuhusu masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na umuhimu wa taaluuma ya hali ya hewa kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii, jambo ambalo lilimpa hamasa ya kujiendeleza katika fani ya hali.

Kwa taarifa zaidi tembelea: www.meteo.go.tz

No comments:

Post a Comment