VETA KANDA YA KATI YATOA MAFUNZO YA UFUGAJI WA MBUZI, KONDOO WILAYA YA IKUNGI BAADA YA KUBAINI SOKO LA UHAKIKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 13 September 2023

VETA KANDA YA KATI YATOA MAFUNZO YA UFUGAJI WA MBUZI, KONDOO WILAYA YA IKUNGI BAADA YA KUBAINI SOKO LA UHAKIKA

Afisa Masoko na Utafiti Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, Sadan Komungoma (katikati) akizungumza na wajasiriamali wakati wa mafunzo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo yaliyoandaliwa na VETA kwa wananchi wa Kata ya Unyahati wilayani Ikungi yaliyofanyika Septemba 13, 2023 Chuo cha VETA Ikungi mkoani Singida. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula na kushoto ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Ladslous William Mwalimu kutoka VETA Singida.

 Na Dotto Mwaibale, Ikungi 

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati inaendelea kutoa mafunzo ya ufugaji wenye tija wa mbuzi na kondoo kwa wajasiriamali wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ili waondokane na ufugaji wa mazoea kwenda kwenye ufugaji wa kibiashara ambao utawakwamua kiuchumi.

 Afisa Masoko na Utafiti VETA Kanda ya Kati, Sadan Komungoma, akizungumza leo Septemba 13, 2023  wakati wa mafunzo hayo kwa wajasiriamali wa Kata za Unyahati Kijiji cha Muungano wilayani Ikungi mkoani Singida alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wananchi kufanya ufugaji wenye tija na kuwapatia masoko ambayo yatawaongezea kipato.

"Mafunzo haya ni ya awamu ya pili kutolewa katika Chuo cha VETA Ikungi tangu kilipozinduliwa mwaka jana yanalenga kuboresha biashara za wananchi ili wafuge mbuzi, kondoo na kuku kwa ubora ambao utaongeza thamani ya nyama na mayai," alisema.

 Komungoma,alisema VETA imeanza kutoa mafunzo hayo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo kutokana na Mkoa wa Singida kuwa na soko kubwa la wanyama hao hasa wakati wa Sikukuu ya Eid al-Adha  ya kuchinja ambapo maelufu ya wanyama hao uchinjwa lakini wakinunuliwa kutoka mikoa mingine baada ya Singida kutokuwa nao wa kutosha.

" Mkoa wa Singida unawaumini wengi wa dini ya kiislam ambao moja ya nguzo yao kuu ni kutimiza ibada ya chinja ya wanyama kama ng' ombe, mbuzi na kondoo ambao kama wangekuwa wanapatikana kwa wingi wasingekuwa wanakwenda kununuliwa mikoa mingine bali wangepatikana hapahapa na kuwa fursa kwa wakazi wa Singida," alisema Komungoma.

Alisema baada ya VETA kufanya utafiti na kubaini kuwepo kwa soko la wanyama hao ndipo wakaja na mpango wa kutoa mafunzo hayo yenye lengo la kubadilisha uchumi wa wana Singida kwa kupitia ufugaji wa wanyama hao ambao hawashambuliwi na magonjwa ya mara kwa mara kama ilivyo kwa wanyama wengine.

Alisema VETA inatoa mafunzo ya muda mfupi  kwa wajasiriamali kwenye mikoa ya kanda ya kati ambayo ni Dodoma,Singida na Manyara ili kuwawezesha wananchi kunufaika na uwepo wa vyuo vya VETA vilivyoanzishwa kila wilaya ili wajikwamue kiuchumi kupitia ujasiriamali na ufugaji.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo aliwataka washiriki kuzingatia yale ambayo watafundishwa kwani ni mafunzo yenye tija na yana kwenda kuinua maisha ya familia na taifa kwa ujumla.

"Hivi sasa ufugaji unafaida sana ukienda Mnadani kule njia Panda mbuzi mmoja anauzwa hadi Sh.200,000 tofauti na bei waliyokuwa wakiuzwa zamani nawaombeni zingatieni mafunzo haya kwani ni ya muhimu sana," alisema Myula.

Aidha, Myula alisema mafunzo hayo ni fursa kwao kwani baada ya kuyapata kutapanua wigo wa utafutaji kwa kuuza mifugo yao, mayai na mazao mengine yanayotokana na wanyama hao na watakuwa wamepata ajira ya kudumu tofauti na ile ya kuajiriwa kwa mtu au Serikalini.

Myula alitumia nafasi hiyo kuwashukuru VETA kwa kutoa mafunzo hayo na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha  fedha kwa ajili ya kuwasaidia watanzania kukuza uchumi wao.

 Washiriki  wamafunzo hayo Mwanahamisi Hamisi, Gangala Nsunaluga, Saida Juma na Sauli Mayele walisema licha ya kuanza ufugaji tangu siku nyingi lakini walikuwa hawajui mbinu za ufugaji wa kisasa wenye tija na kuwa wanaishukuru VETA kwa kuwapa mafunzo hayo.

Mfugaji na mkulima Mariam Ntandu kutoka Kijiji cha Muungano Kata ya Unyahati, Ikungi anasema anamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea Chuo cha Ufundi cha  VETA katika wilaya hiyo na kuwezesha fedha za mafunzo hayo na kuwa shukurani za pekee ziende kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA Kanda ya Kati John Mwanja na watendaji wenzake kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yanakwenda kubadilisha maisha yao kupitia fursa za ufugaji wa kisasa.

Alisema shukurani nyingine zimuendee Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi kwa kuwapelekea wataalam ambao wamekuwa wakiwafundisha mbinu za kilimo na ufugaji bora wa kuku, mbuzi na kondoo.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula  akifungua mafunzo hayo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Ladsilous William Mwalimu kutoka VETA Singida.akitoa mafunzo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo kwa washiriki wa mafunzo hayo.
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Elisha Kitisho akitoa mafunzo ya ufugaji bora wa wanyama hao.
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Penveli Raphaely akitoa mafunzo ya ufugaji bora wa wanyama hao.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wajasiriamali hao, Sauli Mayele akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Mshiriki wa mafunzo hayo Mzee Gangala Nsunaluga akichangia jambo wakati wa mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.

Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.

Mshiriki wa mafunzo hayo Mwanahamisi Hamisi akiuliza swali kuhusu ufugaji wa mbuzi na kondoo.

 Mafunzo yakiendelea.

Picha ya pamoja 


No comments:

Post a Comment