Na WMJJWM, Tarime - MARA
SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeihimiza jamii kote nchini kukumbuka ujenzi wa makazi ya wazee wasiojiweza wakati huu wa mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis wakati akishiriki katika shughuli za maendeleo
Wilayani Tarime mkoani Mara.
Akiwa kwenye ujenzi wa nyumba ya daktari wa zahanati ya Kijiji cha Soroneta amesema Jamii inatakiwa kushiriki katika shughuli za maendeleo ili wawe na umiliki wa miradi hiyo hususan suala la utunzaji ili idumu.
Mwanaidi amesema, Kampeni ya Amsha Ari ni moja ya juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum juu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Jamii ya Mwaka 1996 inayohimiza Wananchi kujitolea wakati wa shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao.
"Mimi nimekuja hapa kuamsha ari ya wananchi kuweza kujenga makazi bora na pia kusaidia watu wengi kuwa na makazi bora hasa wazee wasio na uwezo" amesisitiza Naibu Waziri Mwanaidi.
Naye Diwani wa Kata ya Nyarelo Japheth Marwa, amesema wananchi wa kata hiyo wamekuwa na moyo na ari ya kujitolea katika shughuli za maendeleo na wataendelea kujitoa ili kufanikisha miradi mbalimbali ya huduma za jamii iweze kuwasaidia kuondokana na changamoto zinazowakabili
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kijiji cha Soroneta Kata ya Nyarelo Dkt. Richard Kitende ameishukuru Serikali kwa kuunga mkono juhudi za wananchi kutekeleza miradi ya Maendeleo kwani inasaidia kuwapa moyo wa kujitoa na kusaidia upatikanaji wa huduma muhimu karibu na maeneo yao.
Akizungumzia hatua hiyo, Mbunge wa Tarime Vijijini Mwita Waitara amesema ni jambo jema viongozi kuonesha mfano kwenye masuala ya maendeleo na jamii kwani itasaidia kuwa na moyo na mwamko kwa wananchi kuchangua katika shughuli za maendeleo.
Awali, Afisa Maendeleo ya Jamii Janeth Michael alisema mradi huo umeshirikisha wananchi kwa shughuli za kuchimba msingi, kusomba mawe na kujenga boma ambapo gharama zote za nguvu ya wananchi ni shillingi Millioni 8.1 huku wakiungwa mkono na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime iliyotoa shillingi Millioni 20 kuunga mkono juhudi za Wananchi.
No comments:
Post a Comment