MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameshukuru juhudi zinazochukuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) katika kufanikisha hatua mbali mbali za maendeleo hapa Nchini.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani Jijini hapa, akiongea na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Tanzania anayemaliza muda wake, Bi Shalini Bahuguna, aliyefika hapo kwaajili ya kuagana.
Amesema UN kupitia Mashirika yake wamekuwa wakisaidia na kuhamasisha utekelezaji wa Sera na Mipango mbali mbali ikiwemo ya Kiuchumi na Huduma za Maendeleo kwa jamii, Serikali na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Othman amelitaja Shirika la UNICEF kuwa lipo mstari wa mbele kusaidia Mipango hiyo hapa Nchini, ambayo ni pamoja na Ukuzaji wa Sekta ya Maji Safi, Huduma za Elimu, Afya, Malezi na Maendeleo ya Akinamama na Watoto, na Misaada mbali mbali kwa Jamii ya Watu Wenye Ulemavu.
”Tutakosa mchango wako mkubwa na mikono yenye wepesi wa kusaidia Nchini kwetu, bali matumaini yetu bado yapo kwa hao wanaofuata ambao tunaamini wataendeleza moyo na juhudi hizo hizo”, amesema Mheshimiwa Othman akikumbuka mchango wa Bi Shalini kwaajili ya Maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Aidha, Mheshimiwa Othman ameongeza na kusisitiza akisema, ”ni vigumu kusema ’good-bye’ (kwa-heri) kutokana na machungu ya kuepukana na wale mliojenga mazowea ya kusaidiana kwa muda mrefu, ingawa ’zawadi njema kwa kazi iliyofanikiwa ni kutoa tena fursa ya kuitekeleza vyema”.
Hivyo, licha ya kuahidi kuendeleza mashirikiano baina ya Serikali ya Zanzibar na Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Othman amemtakia kila la kheri Mwakilishi huyo anayemaliza Muda wake wa Utumishi hapa Nchini, na kumuombea mafanikio mema katika safari yake ya maisha huko anakokwenda.
Kwa upande wake Bi Shalini amepongeza juhudi za Mheshimiwa Othman tangu aliposhika Wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais, takriban Miaka Miwili iliyopita, kwa kuleta ufanisi katika mambo mbali mbali ya maendeleo yakiwemo Mazingira, Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya, Ulinzi kwa Watoto na Watu Wenye Ulemavu, pamoja na Mpango wake wa sasa wa ’Green Legacy’, unaolenga kuirithisha Zanzibar ya Kijani kwa vizazi vijavyo.
”Hatuwezi kuipoteza fursa ya kuendeleza jukumu la kuisaidia Zanzibar pamoja na mambo mengi yakiwemo ustawi bora wa jamii kwa kuweka mfano bora wa makuzi ya watoto hapa Visiwani”, ameeleza Bi Shalini.
Katika Ujumbe wake Mwakilishi huyo ameambatana na Maafisa Waandamizi kutoka Shirika la UNICEF Nchini ambao ni Bw. Ahmed Rashid Ali na Bi Laxmi Bhawani.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amefanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa India hapa Nchini, Dr. Kumar Praveen, ambaye amefika huko Migombani, Ofisini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kwaajili ya kujitambulisha.
Katika maongezi hayo, Mheshimiwa Othman ameeleza fungamano la tangu asili kati ya Zanzibar na India, kiasi ambacho hadi sasa kumekuwepo na hata uwiano wa Marejeo (References) katika matumizi ya baadhi ya Sheria za Mahakama, baina ya pande mbili hizo.
Naye, Balozi Praveen ameeleza kuwa hatua yake ya kuja kujitambulisha inathibitisha mahitaji yake ya kuendeleza mashirikiano ya muda mrefu kati ya Serikali ya India na Zanzibar.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Juni 06, 2023.



No comments:
Post a Comment