![]() |
| Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi. |
KATIBU Mkuu wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesisitiza, katika mahojiano maalum na Kipindi cha Jahazi cha Clouds FM kutokea Makao Makuu Dodoma, siku moja tu baada ya Bunge kupitisha kwa asilimia 100 Bajeti ya Wizara hiyo, kuwa katika utekelezaji wa Bajeti hiyo mkazo na nguvu kubwa itaenda katika kuhifadhi na kutangaza utalii.
“Tutahifadhi sana kwa maana lazima tulinde maliasili zetu ambazo ndio vivutio vikubwa tulivyojaaliwa ikiwemo kupambana na tatizo la wanyama wakali na tutatangaza sana kwa sababu kupitia Royal Tour tumeweka viwango na tumeona kuwa tumewekeza kutangaza kwa Bilioni 7 lakini imetulipa kwa kuingiza zaidi ya trilioni 2 kwenye uchumi wa nchi ndani ya mwaka mmoja tu,” alisema Dkt. Abbasi na kuongeza pia kipaumbele maalum na cha kipekee kingine cha sekta hizi kitakuwa katika kuondoa changamoto za kufanya biashara katika sekta ya utalii ili wadau waweze kufanya kazi zao vyema.
“Utalii ni biashara na utalii ni mapato kwa Taifa hivyo lazima sekta hii wadau wake tuwalinde, tuwapetipeti, tuwatetee na tuwe walezi kwao. Sasa uzuri Mhe. Waziri Mohammed Mchengerwa amenitangaza mimi mwenyewe kusimamia mageuzi katika eneo hili. Tutashirikiana na wadau kuliko wakati wowote katika sekta hizi.”


No comments:
Post a Comment