HAKIELIMU WAZINDUWA KITABU KUKOLEZA MJADALA KISWAHILI KUTUMIKA KUFUNDISHIA SEKONDARI, VYUONI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 27 June 2023

HAKIELIMU WAZINDUWA KITABU KUKOLEZA MJADALA KISWAHILI KUTUMIKA KUFUNDISHIA SEKONDARI, VYUONI

Profesa Musambayi Katumanga (wa pili kushoto) wa Chuo Kikuu cha nchini Kenya na mgeni rasmi katika Kongamano la 14 la Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Umajumui wa kiafrica (Pan Africanism) akizinduwa rasmi kitabu cha Hakielimu cha 'Kiswahili - Lugha ya Kufundishia Kikwazo cha Usawa katika Kujifunza na Upimaji Tanzania’. Kulia ni Mwenyekiti wa kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha umajimui wa Africa, Profesa Rwekaza Mukandala na meza kuu wakishuhudia.

Mwenyekiti wa Bodi ya Hakielimu, Richard Mabala akizungumza na washiriki wa Kongamano la 14 la Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Umajumui wa kiafrica (Pan Africanism), Chuo Kikuu cha Dar as salaam linalofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Mhariri wa Kitabu cha Kiswahili - Lugha ya Kufundishia Kikwazo cha Usawa katika Kujifunza na Upimaji Tanzania ambaye pia ni Mshauri Mwelekezi wa Hakielimu, Dk. Wilberforce Meena (kushoto) akimkabidhi nakala ya kitabu hicho Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe Rev. Dk.Benson Bagonza mara baada ya kuzinduliwa.

Mhariri wa Kitabu cha Kiswahili - Lugha ya Kufundishia Kikwazo cha Usawa katika Kujifunza na Upimaji Tanzania ambaye pia ni Mshauri Mwelekezi wa Hakielimu, Dk. Wilberforce Meena (kushoto) katika picha ya kumbukumbu na Mwenyekiti wa kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha umajimui wa Africa, Profesa Rwekaza Mukandala (kulia) mara baada ya kuzinduliwa.

Na Joachim Mushi, Dar

TAASISI ya Hakielimu imezinduwa kitabu kinachojenga hoja na kuchochea matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Tanzania inaweza kutumika kama lugha ya kufundishia kwenye ngazi ya shule za sekondari pamoja na vyuo vikuu.

Kitabu hicho kimezinduliwa jijini Dar es Salaam na Profesa Musambayi Katumanga wa Chuo Kikuu cha nchini Kenya mgeni rasmi katika Kongamano la 14 la Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Umajumui wa kiafrica (Pan Africanism), Chuo Kikuu cha Dar as Salaam.

Akizungumzia kitabu hicho mara baada ya kuzinduliwa, Mhariri wa Kitabu na Mshauri Mwelekezi wa Hakielimu, Dk. Wilberforce Meena allisema kitabu hicho kinazungumzia jinsi ambavyo Tanzania kwa sasa inaweza kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, hasa katika ghazi ya Shule za Sekondari na Elimu ya juu.

Alisema kuwa, kitabu hicho kilichopewa jina la ‘Kiswahili - Lugha ya Kufundishia Kikwazo cha Usawa katika Kujifunza na Upimaji Tanzania’ kimejumuisha makala anuai zilizoandaliwa na wataalam waliobobea katika lugha, ambao wameelezea jinsi ambavyo Kiswahili kwa wakati huu kimefikia uwezo wa kutumika kama lugha ya kufundishia katika shule na vyuo vyetu nchini Tanzania.

“…Tunafikiri kuwa kwa kuzinduwa kitabu hiki na haswa kwa wale watakaopata muda wa kukisoma kitazidi kuwapanua, kuwaonesha jinsi ambavya sisi kama nchi tunaweza kutumia Kiswahili katika elimu yetu…kumekuwa na mjadala kwa muda mrefu juu ya matumizi ya Kiswahili na lugha ya kiingereza katika kufundishia, lakini kitabu hiki kinajaribu kujibu maswali ya mjadala huu kwa kiasi kikubwa sana” alisema Dk. Meena ambaye pia ni Mhariri wa kitabu hicho.

Akifafanua zaidi Dk. Meena alibainisha kuwa makala katika kitabu hicho zinaonesha wazi kuwa mpaka sasa Tanzania imechelewa katika kufanya maamuzi juu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili kufundishia hasa ngazi ya sekondari na vyuoni. “..kimsingi wakati umefika sasa wa kuanza kukitumia Kiswahili kufundishia katika elimu yetu ya sekondari na elimu ya juu,” alisema.

“Kitabu hiki ni msaada mkubwa kuendelea kujenga hoja hasa kwa watetezi wa lunga ya Kiswahili nchini kwenye mjadala unaoendelea juu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili kutumika kufundishia kwenye ngazi ya shule za sekondari na vyuoni.

Aidha akijibu hoja ya kwamba huenda lugha hiyo ikashindwa kujitosheleza kimsamihati alisema lugha hiyo inajitosheleza na ni jambo la kawaida lugha kutohoa maneno kutoka lugha nyingine pale inapobidi.

Pamoja na hayo aliongeza kwamba Kiswahili kinajitosheleza na kuungwa mkono, kwani hata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (UDSM) hapo nyuma waliwahi kuandika vitabu vya Kiswahili kwa masomo ya Sayansi kwa ajili ya matumizi ya shule za sekondari.

“Kiswahili kinajitosheleza katika kutumika kufundishia na bado kuna fursa hata ya kuendelea kutohoa baadhi ya maneno  kutoka katika lugha nyingine pale inapobidi, kwani hata kiingereza kinachotumika kwa sasa yapo maneno mengi yametoholewa kutuka katika lugha zingine,” alisisitiza mhariri huyo wa kitabu.

No comments:

Post a Comment