RAS SINGIDA : WALIMU KUTOA MATOKEO MAZURI YA UFAULU WANAFUNZI SI HIYARI NI LAZIMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 25 May 2023

RAS SINGIDA : WALIMU KUTOA MATOKEO MAZURI YA UFAULU WANAFUNZI SI HIYARI NI LAZIMA

Katibu Tawala Mkoa wa Singida (RAS), Dk.Fatma Mganga, akizungumza wakati akifungua mkutano wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Kanda ya Kati wa mikoa ya Dodoma na Singida mjini Singida leo May 25, 2023.

Na Dotto Mwaiale, Singida

KATIBU Tawala Mkoa wa Singida (RAS), Dk.Fatma Mganga amesema suala la walimu kutoa matokeo mazuri ya kufaulu wanafunzi sio jambo la hiyari bali ni lalazima.

Maganga ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo leo May 25, 2023 wakati akifungua mkutano wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Kanda ya Kati wa mikoa ya Dodoma na Singida wenye lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kitaaluma ambapo walimu wakuu wapya  walioteuliwa hivi karibuni walitambulishwa.

"Katika suala hili la kufaulu wanafunzi na kutoa matokeo mazuri ni lalazima tutalisimamia kwa karibu hatutalifanyia mchezo. Kumekuwa na kauli moja hivi kuwa sisi tupo kwenye utumishi wa umma na ni wafanyakazi wa kudumu kauli hii wakati mwingine huwa haitumiki vema, nifanye vizuri au vibaya kwangu haijalishi mimi ni muajiriwa labda niwe na makosa ya kukiuka maadili lakini hili la kutoa matokea mazuri sio la lazima kwangu," alisema Mganga.

Mganga alisema kauli hiyo kwa mtumishi wa umma sio nzuri kwani wapo kwa ajili ya kufanya kazi ambapo aliwasihi wakuu hao wa shule kwenda kufanya kazi kwa bidii na kusimamia utoaji wa matokeo mazuri ya ufaulu wa wanafunzi.

Alisema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji wa kuogopesha katika sekta ya elimu kwa kutoa fedha nyingi na matarajio ni kupata matokeo mazuri.

Alisema hivi karibuni Mkoa wa Singida umepokea Sh. Bilioni 9.2 kwa ajili ya kuboresha shule za msingi na juzi wamepokea zaidi ya Sh.Bilioni 3 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa kwenye shule za sekondari hivyo kila mmoja anapaswa kujua mahitaji ya saerikali ni yepi kwa kufanya uwekezaji huo mkubwa katika sekta hiyo wakati kuna sekta nyingi ambazo ingeweza kupeleka fedha hizo.

Aidha, Mganga aliwataka wakuu hao wa shule kwenda kuendelea kusimamia maadili ya wanafunzi na walimu katika maeneo yao kwani wao ndio wanaotegemewa katika jambo hilo.

Pamoja na hilo Mganga aliwataka wakuu hao kwenda kusimamia vizuri miradi mbalimbali inayofanyika kwenye shule zao baada ya serikali kutoa fedha nyingi na kuwa ifanyike kwa thamani iliyopangwa na kwa viwango vinavyokubalika na wasishawishike kuchua hata senti moja kuepuka kuja kuumbuka.

Pia aliwataka wakuu hao wa shule kwenda kuhimiza na kusimamia michezo mbalimbali mashuleni.

Akielezea njia itakayosaidia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi alisema kila mwalimu awe anafanyiwa tathmini ya masomo yake anayoyafundisha na kuwa jambo hilo liwe linafanyika mara kwa mara.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari (TAHOSSA) Kanda ya Kati, Jeremia Kitiku alisema wakati wote mikutano ya namna hiyo inapofanyika ajenda yao kubwa ni kujadili mbinu za ufaulu wa wanafunzi na changamoto zilizopo kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa TAHOSSA Kanda ya Kati kwenda Taifa, Peter Mlugu alisema mkakati wao ni kwenda kuondoa kabisa ufaulu wa daraja la nne na ziro na kutekeleza yale yote aliyoyaelekeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk.Mganga kuyafanya.

Naye Katibu wa TAHOSSA Kanda ya Kati, Benedict Dau alisema mkutano huo umewahusisha viongozi mbalimbali wa sekta ya elimu wakiwemo kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) ambao walitoa mada iliyohusu namna gani ya kutunga maswali ya kupima umahiri wa wanafunzi.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Dk. Crispin Ryakitimbo akizungumza katika mkutano huo alisema watatoa mafunzo kwa wakuu wapya wa shule za sekondari walioteuliwa ambayo yatahusu masuala mbalimbali yakiwepo ya uongozi na utawala.

Mafunzo hayo yalihusisha wakuu wa shule za Sekondari kutoka halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma ambazo ni Dodoma Jiji, Chemba, Chamwino, Bahi, Kongwa, Mpwapwa, Kondoa DC na Kondoa TC na kwa Mkoa wa Singida ni halmashauri saba za Itigi, Ikungi, Mkalama, Iramba, Manyoni, Singida DC na Singida Manispaa.

Viongozi wakiwa meza kuu. Kutoka kulia ni Mwakilishi wa TAHOSSA Kanda ya Kati kwenda Taifa, Peter Mlugu, Makamu wa Rais wa TAHOSSA, Juliana Limbe, Katibu wa TAHOSA Kanda ya Kati, Benedict Dau, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga na Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Kanda ya Kati, Jeremia Kitiku

Viongozi wakishiriki kuimba wimbo wa Taifa.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Kanda ya Kati, Jeremia Kitiku, akizungumza katika mkutano huo.
Mwakilishi wa TAHOSSA Kanda ya Kati kwenda Taifa, Peter Mlugu, akizungumza kwenye mkutano huo.
Katibu wa TAHOSA Kanda ya Kati, Benedict Dau, akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa TAHOSSA, Mkoa wa Singida, Paskal Kichambati akiongoza mkutano huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida Dk. Crispin Ryakitimbo akizungumza katika mkutano huo.
Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Taswira ya mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Taswira ya mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Taswira ya mkutano huo kwa nyuma.
 

No comments:

Post a Comment