KWANINI TUMFIKIRIE MZEE WETU MALECELA...? - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 16 May 2023

KWANINI TUMFIKIRIE MZEE WETU MALECELA...?

Ndugu zangu,

MZEE wetu John Malecela, ndani ya miaka miwili amewapoteza watoto wake vipenzi wawili. Mwaka jana amemzika binti yake kipenzi, Mwele Malecela.

Mwaka huu kule kwao Mvumi anakwenda kumzika mwanawe kipenzi William Malecela.

Jioni hii nimefika nyumbani kwa Mzee Malecela pale Kilimani, Dodoma. Nimepata nafasi ya kumpa mkono wa pole na kuzungumza naye mawili matatu.

Kwa kumwangalia usoni niliona uso wa huzuni kuu aliouvaa.

Kwa wale wa kizazi changu tutakumbuka pia pigo alilolipata Mzee wetu Malecela miaka ile ya 90. Alimpoteza kijana wake kipenzi pia, Ipyana Malecela. Huyu Ipyana tuliyemwona pia akichanua kwenye siasa za Umoja wa Vijana CCM akawa kama moto mkali uliozimika ghafla bila hata kuacha moshi. Kwangu, Ipyana, au ‘ Ipi Malecela’ kama tulivyomfahamu zaidi kwa jina hilo, alikuwa ndiye haswa aliyejiandaa kuvaa viatu vya Baba yake kwenye Uongozi wa Kisiasa na Kiserikali.

Hakika, mwanadamu usiombe yakufike, maana, hakuna jambo gumu kwenye maisha ya mwanadamu kama mzazi kumzika mtoto wako wa kumzaa. 

Katika wakati huu mgumu kwake na kwa familia yake ya karibu, na nikiwa kama mzazi pia, fikra  zangu nazielekeza kwa Mzee wetu Malecela na familia yake ya karibu akiwamo Mama Anne Malecela. Ni mwanamama anayemuhitaji zaidi ubavuni mwake katika wakati huu.

Na hakika, William niliyemfahamu mimi si yule wa mitandaoni. Nilimfahamu kabla ya umaarufu wa mitandaoni. Ni William kila nilipokutana nae stori zetu, ukiacha mambo ya msingi ya kitaifa, ilikuwa ni pamoja na kwa mfano, William angeniuliza;

“ E bwana Maggid, nasikia huko Iringa kilimo cha parachichi kinalipa, ikoje lakini?”

Apumzike Kwa Amani na pole nyingi kwa Mzee wetu Malecela, ndugu, jamaa na marafiki.

Maggid Mjengwa.

Dodoma.

No comments:

Post a Comment