BODI ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB) iameahidi kuendeleza ushirikiano na Bodi ya Usajili wa Wahandisi ya Kenya (EBK), katika mkataba wa makubaliano ya pamoja waliyoweka ili kuhakikisha wanakidhi vigezo vya ushindani katika nchi za umoja wa Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa kufunga warsha ya wiki moja iliyoandaliwa na ERB, jijini Dodoma, Msajili wa Bodi hiyo, Eng. Benard Kavishe, amesema kuwa dhumuni la warsha hiyo ni kuboresha mazingira katika taaluma hiyo ambapo itasaidia mhandisi kutoka Tanzania, Kenya pamoja na wale walio katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutambulika na kufanya kazi katika nchi hizo bila ya vizuizi vyovyote.
“Haya ni makubaliano ambayo tuliafikiana tangu mwaka 2012, lengo likiwa ni kuwasaidia wahandisi waliosajiliwa katika nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweza kufanya shuguli zao bila vizuizi na pia kukutana na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu ili wote kuwa na viwango vinavyofanana”, amesema Eng. Kavishe.
Aidha, Eng. Kavishe amefafanua kuwa tangu makubaliano hayo kuafikiwa kumekuwa na ziara na warsha za mara kwa mara kwa wahandisi hao ambapo kwa mwaka huu warsha ya kujengea uwezo wataalamu hao imefanyika jijini Dodoma.
Ametaja baadhi ya vigezo vilivyomo katika makubaliano yao ikiwa ni pamoja na kuwa na viwango sawa katika ufundishaji,usajili na kuwalea hali itakayorahisisha utendaji kazi na kufungua ajira katika nchi za Afrika Mashariki.
“Tulipokea ugeni wa watu Tisa kutoka Kenya ambao wamekuja kujifunza na kubadilishana uzoefu kati yetu ambapo tulichukuwa kutoka kwao kile ambacho hatuna na kile ambacho hawana wamechukua kwetu”, amesema Eng. Kavishe.
Ameongeza kuwa baada ya ziara hiyo kumalizika anaamini kuwa wahandisi wa Tanzania na Kenya watafanana katika viwango vyao vya kiutendaji na hivyo kuendeleza ushirikiano na kuwa na ushindani dunia nzima.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Bodi ya Usajili ya Kenya (EBK), Margaret Ogai, amesema kuwa kupitia warsha hiyo wamejifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja kuwa na utaratibu wa kufanya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaotoka vyuoni ambao wamesoma taaluma ya kihandisi, kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kusaidia wahandisi katika kuwapeleka mafunzo ya kuwajengea uwezo na kusajili wahandisi wengi wakike chini ya miaka 35.
Naye, Mhandisi kutoka Kenya ambaye ni mmoja wa washiriki wa warsha hiyo, Monica Wangari, amesema kuwa warsha hiyo imesaidia kujua masuala mengi ambayo anaamini kwa namna moja ama nyingine yataenda kufungua fursa ya ajira kwa wahandisi wengi wa Tanzania na Kenya pamoja na wale walio katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maendeleo yaliyofanyika katika jiji la Dodoma ambapo licha ya mafunzo waliopata katika warsha hiyo pia walipata fursa ya kutembelea Mji wa Serikali, eneo la Mtumba, Dodoma na kuona namna ulivyopangika na kuvutia.
Mhandisi Veronica Ninalo kutoka ERB, ambae ni Mshiriki kutoka Tanzania uandaamesisitiza kwa Serikali kupitia Bodi hiyo kuandaa warsha za mara kwa mara ili kubadilishana uzoefu kutoka sehemu mbalimbali ili kuimarisha na kuboresha taaluma hii.
Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya pamoja katika nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuendeleza na kukuza taaluma ya uhandisi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
No comments:
Post a Comment