Muonekano wa moja ya kituo cha mabasi yaendayo
haraka eneo la TAZARA ambacho ujenzi wake unaendelea.
IMEELEZWA takriban miradi 16 ya ujenzi wa barabara yenye gharama ya shilingi trillion 1.4, sawa na kilomita 603 inaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini katika kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii zinaendelea kuimarika na kuleta tija kwa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema hayo leo wakati
akikagua maendeleo mradi wa barabara ya Mabasi yaendayo Haraka BRT III jijini
Dar es Salaam.
Eng. Mativila ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Barabara ya Mianzini-Olemringaringa-Sambasha KM 18, Ntendo-Muze-Kilyamatundu KM 179, na Malagarasi-Ilunde-Uvinza KM 51.1.
Mingine ni Barabara ya Karatu-Mbulu-Hydom-Sibiti-Lalago-Maswa KM 389, Matai-Kasesya KM 50, Ntyuka-Mvuni KM 76 na barabara ya Tarime-Mugumu KM 87.14.
Eng. Mativila amesema
Serikali inatambua umuhimu wa barabara za lami na madaraja ya kisasa katika
kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote na hivyo kuleta tija katika
shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ujumla.
"Nawahakikishia
wakazi wa Dar es salaam Barabara ya BRT II, na BRT III zitakamilika kwa mujibu
wa mpango tuliouweka ili kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katikati jijini
la Dar es Salaam," amesisitiza Eng. Mativila.
Aidha amewataka
mameneja wa TANROADS nchini kote kuhakikisha barabara zinapendezeshwa na kuwa
katika hali bora wakati wote.
Kwa upande wake Meneja
wa barabara za BRT Eng. Barakaeli Mmari amesema wamejipanga kuhakikisha magari
yanaongozwa vizuri katika barabara zinazojengwa ili kupunguza msongamano wa
magari na kuepuka ajali.
No comments:
Post a Comment