DENIS MDOE; MWANASOKA ALIYEFUNGAMANISHA ELIMU NA MICHEZO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 27 April 2023

DENIS MDOE; MWANASOKA ALIYEFUNGAMANISHA ELIMU NA MICHEZO

 

Dennis Mdoe.

Na Adeladius Makwega, MWANZA

“NIMEPOKEA taarifa ya masikitiko makubwa kuwa mwanafamilia mwenzetu Dennis Mdoe, aliyesoma Tambaza mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hesabu (PCM) kati ya mwaka 1981-1983 amefariki ghafla usiku wa kuamkia Aprili 24, 2023 huko Arusha.”

Huo ukiwa ujumbe uliotumwa kwa wanafunzi waliosoma Tambaza miaka mbalimbali na ulimfikia Mwanakwetu saa 9.26 siku hiyo hiyo, ukitumwa na ndugu Samweli Ruhuza ambaye ni miongoni mwa wanafunzi wa enzi hizo waliosoma shuleni hapo. Kwa hakika tangu mwaka 1983 hadi leo hii ni miaka 40 ambao ni umri wa mtu mzima mwenye watoto kadhaa na hata hao watoto hao wana watoto.

Ukweli uliowazi jina DENNIS MDOE walio wengi hawalifahamu kabisa. Shida mojawapo ya mchezo wa soka siyo muziki, ukiacha muziki rekodi zako zitaendelea kuchezwa lakini mpira pale unapotundika jozi za viatu begani, ndiyo basi tena. Watakukumbuka wale uliokuwa nao na rika lako. Hilo ndiyo chanzo leo hii jina la Dennis Mdoe linaonekana kama ni geni katika ulimwengu wa mashabiki wa soka vijana wa Tanzania.

Wingu hilo la kutomfahamu mwamamichezo huyu hodari wa Tanzania limemuhamasisha Mwanakwetu kuwatafuta wale wanafunzi waliosoma naye Tambaza na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kumuelezea mwanasoka huyu mahiri aliyechezea timu mbalimbali.

Dennis Mdoe mchezaji aliyecheza nambari 5, 6, 8 na 10, kwanza alichezea na timu ya shule ya Tambaza alafu Nyota Nyekunde, Ruvu Stars, Timu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars). Nyota Nyekundu ilikuwa ni timu ndugu na Simba ya Dar es Salaam iliyokuwa na makao yake makuu mtaa wa Kongo, baadaye Dennis Mdoe alichezea Young African yenye makao yake makuu Jangwani.

Swali linaloibuka sasa ni ilikuwaje Dennis Mdoe alichezea Nyota Nyekundu aende Yanga badala ya Simba/ Je hakuwa na mapenzi na Simba? Wale waliosoma naye wanasema wazi kuwa kwa wakati ule ilikuwa ngumu mno mchezaji mwenye mapenzi na timu Simba/ Yanga kucheza timu asiyo na mapenzi nayo, maana walikuwa wanachunguza sana kuogopa kusalitiwa mchezoni. 

Expedito Dickens Simmon aliyesoma naye Tambaza kipindi hicho akiwa kidato cha tatu huku marehemu Dennis Mdoe akiwa Kidato cha tano anasema ,

“Dennis alikuwa ni mmojawapo wa wachezaji wachache waliokuwa na akili nyingi darasani, pale Tambaza akisoma PCM yeye na Senyagwa John Samwel Malecela,-mtoto wa John Malecela aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, mwaka 1983 Mdoe na Malecela walifanya vizuri mno kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita kwenye mchepuo wao kitaifa na kuleta gumzo katika mchepuo huo wa PCM.”

Dennis Mdoe alipohitimu kidato cha sita alikwenda JKT Ruvu na huko waliokwenda nae wanadai kuwa yeye ndiye aliyeimarisha mno timu ya soka ya Ruvu Stars. Mafunzo ya JKT yalimalizika huku ikidaiwa kuwa wale waliochaguliwa kusoma sayansi chuo kikuu na wasichana walikaa muda mchache JKT lakini wengine walibakia JKT kwa miaka miwili. Dennis Mdoe alikwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea Shahada ya Uhandisi.

Kwa upande wake Philemon Kelvin Felix ambaye alisoma Tambaza na baadaye kukutana na Dennis Mdoe Chuo Kikuu anasema haya anasema.

“Huyu ndugu yetu Tambaza hatukuwai kukutana kabisa ila tulikuja kukutana naye Chuo KIkuu cha Dar es Salaam, yeye akisoma shahada ya kwanza ya uhandisi na mimi nikisoma shahada ya kwanza ya uchumi. Nakumbuka kuna wakati pale UDSM mkahawani kulikuwa na mapishi ya chakula ambayo hayakuwapendeza wanachuo wengi tukawa tunakwenda kula naye nje pale Survey.”

Kwa maelezo ya mchumi Philemon Felix yanatoa picha muhimu sana kuwa japokuwa Dennis Mdoe alikuwa mwanamichezo bora wa soka, pia alikuwa kijana mpenda elimu na aliyefaulu kwa kiwango kizuri. Ndugu huyu anasema wazi kuwa anakumbuka hata katika timu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dennis Mdoe alicheza na wenzake kadhaa kama vile Charles Gaspar (alichezea pia Young African), Mtemi Ramadhani Mangi (Simba) Colonel Idd Omary Kipingu, Leodgard Chiller Tenga, Shah Hanzuruni huku magolikipa wao walikuwa ni Jaji Francis Mutungi ambaye alikuja kuwa msajiri wa vyama vya siasa na Andrea Maro ambaye alikuwa ni mdogo wa Mama Anna Mkapa.

Ndugu Felix ambaye sana ni mchumi mstaafu anasema kwamba walipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dennis Mdoe akiwa mchezaji wa chuo mambo yote ya michezo ya wanachuo yalikuwa yanasimamiwa na Charles Kitwanga ambaye baadaye alikuja kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,

“Dennis Mdoe alianza kucheza Nyota Nyekundu na siyo African Sports kama wengine wanavyonukuu, alipotoka Nyota Nyekundu ndiyo akaenda Yanga na siyo kutoka Yanga alafu kwenda Nyota Nyekundu. Mtu hawezi kutoka Jeshi la wananchi la Tanzania alafu aende mgambo, mtu ananza mgambo alafu ndipo anakwenda Jeshi la Wananchi.”

Wanafunzi wa Tambaza wa zamani wanasema kuwa Dennis Mdoe alicheza na wachezaji wengi wenye majina makubwa kama vile Lawrence Mwalusako akiwa Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania. 

Mwanakwetu aliuliza, Je Dennis Mdoe alivyokuwa anacheza uchezaji wake unaweza kuulinganisha na mchezaji gani?Ndugu Philemon Felix alikuwa mzito kulijibu swali hilo huku akisema wazi kuwa sasa yeye ni mzee na amelalia upande fulani, lakini anaweza kumlinganisha Dennis Mdoe na wachezaji wa Ulaya si wa Tanzania ya sasa,

“Pale Uingereza, hawa Livepool walikuwa na mchezaji anaitwa Steven Gerald anafanana fika na uchezaji wa marehemu Dennis Mdoe, kwa Tanzania ya zamani ninaweza kumlinganisha labda kidogo na Deo Njohole.”

Hayati Dennis Mdoe alifanya kazi Tanzania alafu alikwenda Botswana, akatoka huko na kwenda Canada, huko alikaa kwa miaka mingi alafu akahamia Qatari. Alirudi Tanzania akafanya kazi na Kilombero Sugar kama mhandisi , hivi karibuni alikwenda Arusha ndipo umauti umemkuta huko.

Wakati Dennis Mdoe anafariki dunia, mama mkewe wake alikuwa amefariki siku chache huko nchini Kenya, huku mkewe akiwa huko Kenya katika maandalizi ya mazishi, nayeye ndugu huyu Dennis Mdoe alikuwa anajianda kwenda kumzikia mkwewe hapo ndipo umauti ukamfika. Mwanakwetu kwa kiasi sasa unaweza kumsilimua nduguyo juu ya mwanasoka na mhandisi Dennis Mdoe kama yalivyo hapo juu, Mwanakwetu upo?

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Marehemu Dennis Mdoe kama alivyosimuliwa hapo juu alikuwa mchezaji soka alikwenda shule na kufanya vizuri katika viwango vya juu, picha hiyo inatoa taswira moja kubwa kuwa ni jambo la msingi sana kama watoto wetu wataambatanisha ushiriki wao katika michezo na taalumu zao. 

Dennis Mdoe maiti yake inapoingizwa kaburini inaambatana na uanasoka wake bora wa Tanzania katika Timu ya Taifa (Taifa Stars) ambapo ameichezea mechi kadhaa, isitoshe pia anazikwa akiwa miongoni mwa wahandisi wa Tanzania waliowahi kufanya kazi hapa nyumbani na ughaibuni.

Wanafalsafa kadhaa wa elimu kama John Dewey, Aristotle na Plato wanatilia maanani kufungamanisha ushindani wa michezo na elimu, hilo lina manufaa makubwa hata pale nguvu za uchezaji zinapokwisha kwa mwanamichezo wetu taaluma yake inatumika kulijenga taifa lake, pia michezo hiyo inasaidia kuongeza ushindani darasani , huku akili na mwili wa mwanafunzi kuwa vizuri kujifunza.

Makala haya yanatoa pole kwa marafiki zake wote, yanatoa pole kwa walisoma nae tangu Tambaza hadi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yanatoa pole kwa jamaa wote, marafiki na kwa wapenzi wote wa soka la Tanzania. Mwanakwetu anaweka chini kalamu yake akisema kuwa Buriani Dennis Mdoe- mwanasoka aliyefungamanisha elimu na michezo.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


No comments:

Post a Comment