UTANGULIZI
Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (Tanzania Meteorological Authority -TMA) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 kupitia Tangazo la Serikali GN.459 la tarehe 14 Juni, 2019.
Kabla ya hapo, majukumu ya Mamlaka hii yalikuwa chini ya uliokuwa Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania (Tanzania Meteorological Agency) uliyoanzishwa kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997. Wakala ulichukua nafasi ya iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa (Directorate of Meteorology) ambapo zote Wakala na Idara Kuu zilikuwa na wajibu wa kutoa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mabadiliko hayo ya sheria yameiongezea Mamlaka majukumu ya kudhibiti masuala yote ya hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kuhakikisha miongozo yote ya kitaifa na kimataifa inazingatiwa kwa manufaa ya wadau wa hali ya hewa na Taifa kwa ujumla.
Dira na Dhamira ya TMA
Dira ya TMA
Kuwa kitovu bora cha huduma za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
Dhamira ya TMA
Kuhakikisha uwepo wa huduma bora na za uhakika za hali ya hewa, zinazokidhi matarajio ya wadau kupitia utoaji na udhibiti wa huduma za hali ya hewa kwa usalama na maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.
MAFANIKIO YA HUDUMA ZA HALI YA HEWA
Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huduma za hali ya hewa nchini zimeendelea kuboreshwa na kuimarishwa katika maeneo mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya watumiaji Kitaifa na Kimataifa. Uboreshaji huo umejikita katika kuboresha miundombinu ya hali ya hewa ikiwemo ununuzi wa mitambo na vifaa vya kisasa vya uangazi wa hali ya hewa, ununuzi wa Rada za hali ya hewa; utekelezaji wa mfumo wa kudhibiti ubora wa huduma (Quality Management System); kujenga uwezo kwa watumishi; kuboresha miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo mkoani Kigoma; kuiwakilisha nchi kikanda na kimataifa katika masuala ya hali ya hewa; na kuboresha utoaji wa huduma kwa lengo la kukidhi mahitaji ya sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Maboresho mengine ni katika utekelezaji wa sheria, uboreshaji wa mazingira ya kazi na kukidhi viwango vya kimataifa.
Katika kipindi cha miaka miwili, Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 50 katika bajeti ya maendeleo kwa ajili ya ununuzi wa Rada za hali ya hewa, kununua vifaa vya hali ya hali ya hewa, ukarabati wa vituo vya hali ya hewa pamoja na ujenzi wa Kituo cha Hali ya Hewa cha Kanda ya Mashariki.
Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya hali ya hewa hapa nchini katika masuala yaliyoainishwa ni kama ifuatavyo:-
Uboreshaji wa Miundombinu
Mamlaka ilinunua Rada nne (4) za hali ya hewa ambapo ufungaji wa Rada mbili (2) katika mikoa ya Kigoma na Mbeya unaendelea. Aidha, utengenezaji wa Rada nyingine mbili (2) kiwandani nchini Marekani umefikia asilimia 63. Kukamilika kwa Rada hizi nne (4) za hali ya hewa kutakamilisha lengo la muda mrefu la TMA kuwa na Rada saba (7) za hali ya hewa kwa nchi nzima.
Kielelezo 1: Sehemu ya majengo ya eneo litakalofungwa rada Mbeya .
Mamlaka imefanikiwa kununua kompyuta ya kisasa yenye uwezo mkubwa (Computer Cluster) ambayo itaongeza uwezo wa Mamlaka katika kuchakata,kuchambua taarifa nhingi za hali ya hewa kwa muda mfupi na hivyo kuongeza uwezo wa Mamlaka wa kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa haraka,ushahihi na kuboresha utabori wa maeneo madogo madogo.
Kielelezo 2: Kompyuta kubwa ya Kisasa ya kuchambua data za hali ya hewa (Computer Cluster).
Mamlaka imeendelea na uboreshaji wa miundo mbinu ya vifaa vya hali ya hewa kuendana na teknolojia na matakwa ya kimataifa ikiwemo kuondoa vifaa vyote vinavyotumia zebaki kwa kununua vifaa 15 vya kidigitali vya kupima mgandamizo wa hewa na vifaa 25 vya kidigitali vya kupima joto hewa.
Katika kubiresha huduma za usalama katika usafiri wa anga , Mamlaka imenunua vifaa vya kisasa vya hali ya hewa vitakavyofungwa katika njia ya kuruka na kutua ndege katika viwanja vya ndege vya Abedi Karume-Zanzibar, JNIA-Dar es Salaam, KIA-Kilimanjaro na Songwe.
Mamlaka ilinunua seti tano (5) za vifaa vya utambuzi wa matukio ya radi (Lighting detectors) ambavyo vimefungwa katika maeneo ya Musoma, Mwanza, Bukoba, Tabora na Kibondo mkoani Kigoma na Mamlaka imeendelea na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya hali ya hewa ikiwemo mitambo sita (2) ya kupima hali ya hewa inayojiendesha yenyewe inayohamishika (mobile Automatic Weather Stations).
Kielelezo 3: seti moja ya vifaa vya kutambua matukio ya radi katika kituo cha Kibondo, mkoani Kigoma
Kielelezo 4: Mtambo wa kupima hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga
Kuongezeka kwa viwango vya usahihi
Katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, viwango vya usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kwa ujumla vimeongezeka na kufikia asilimia 88.5, ambapo katika msimu wa mvua za Vuli 2022, viwango vya usahihi vilikuwa asilimia 94.1. Viwango hivi ni juu ya kiwango cha usahihi wa utabiri kinachokubalika na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) cha asilimia 70. Ongezeko hili la usahihi wa utabiri unazifanya huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini kuwa za uhakika na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta zote za kiuchumi na kijamii nchini zinazotegemea hali ya hewa. Kuongezeka kwa usahihi wa utabiri kumetokana na jitihada za serikali kuwekeza katika kusomesha wataalam wa hali ya hewa, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya kuandaa utabiri pamoja na kuongezeka kwa mtandao wa vituo vya kupima hali ya hewa.
Aidha, Mamlaka imeendelea kutoa utabiri wa msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa kwa usahihi na ubora hivyo kuchangia kupunguza athari kwa watu na mali zao. Mfano: mnamo mwezi Oktoba 2021 Mamlaka ilitoa utabiri wa msimu wa mvua za Vuli kuwa chini ya wastani. Utabiri huo uliziwezesha Mamlaka mbalimbali kufanya maamuzi stahiki na kusaidia kuepusha madhara makubwa ambayo yangeweza kutokea.
Huduma za Hali ya Hewa kwa ajili ya shughuli za utunzaji wa Mazingira
Mamlaka imeendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) katika kutekeleza majukumu ya sekta ya hali ya hewa kwa shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwemo kufuatlia mabadiliko ya hali ya hewa yanayopelekea mabadiliko ya tabia nchi.Vituo vya kupima uchafuzi wa hewa (air pollution monitoring 20 vilinunuliwa na kufungwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuona kwa kiasi gani shughuli za kibinadamu zinavyoharibu mazingira. Taarifa za hali ya hewa pia zimekuwa zikitumika katika kufanya upembuzi yakinifu wa athari za miradi katika mazingira (Environment Impact Assessment) na hivyo kusaidia katika utunzaji wa mazingira.
Matumizi ya TEHAMA kuboresha huduma
Mamlaka imetumia fursa ya kukua kwa TEHAMA kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma na pia kurahisisha usambazaji wa taarifa za hali ya hewa;
Mamlaka ilinunua vifaa na mitambo mbalimbali ya kupima hali ya hewa ambayo utendaji wake umerahisishwa kwa kutumia TEHAMA na hivyo kuweza kupima na kutuma taarifa za hali ya hewa katika Kituo Kikuu na Utabiri (CFO) vyenyewe;
Ubunifu wa watumishi wa TMA katika TEHAMA umefanikisha kuundwa kwa mifumo mbalimbali iliyorahisisha shughuli za uendeshaji na utoaji wa huduma. Baadhi ya mifumo hii ni “Meteorological Aviation Information system (MAIS)” ambao imeendelea kuboreshwa na unatumika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa usafiri wa anga; “Marine Meteorological Information System (MMIS) ambao unatumika katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa Bahari ya Hindi na Maziwa Makuu pamoja na “Digital Meteorological Observatory (DMO)”, mfumo ambao unatumika katika kurekodi taarifa za uangazi, kuzituma Kituo Kikuu cha Utabiri wa hali ya hewa. Mifumo hii ya TEHAMA pia imeiwezesha Mamlaka kutoa huduma mahsusi kwa sekta mbalimbali zikiwemo za madini, usafiri wa barabara, ujenzi na utalii.
Kielelzo 5: mwonekano wa mfumo wa kutoa huduma za hali ya hewa kwa usafiri wa kwenye maji (MMIS)
Mifumo mingine iliyobuniwa na wataalam wa Mamlaka ni ile ya mawasiliano ya data kutoka vituoni hadi Kituo Kikuu cha Utabiri na usajili wa vituo vya hali ya hewa na “Regional Specialized Meterorological Center- Dar es Salaam-RSMC Portal” kwa ajili ya Kituo cha Kanda cha kutoa mwongozo wa utabiri kwa Nchi za Ukanda wa Ziwa Victoria;
Utekelezaji wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
Kanuni za Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na.2 ya mwaka 2019 zimekamilika katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na hivyo kuimarisha shughuli za udhibiti, uratibu na utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini pamoja na kupatikana kwa vyanzo vipya vya mapato. Ukusanyaji wa mapato utaiwezesha Mamlaka kupunguza gharama kubwa za uendeshaji kutoka serikalini sambamba na kuendeleza uboreshaji wa huduma za hali ya hewa nchini.
Uboreshaji wa mazingira ya kazi
Katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka imefanikiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa kukarabati vituo saba (7) vya hali ya hewa vilivyopo katika mikoa ya Singida, Songwe, Mpanda, Shinyanga, Songea, Mahenge na Tabora pamoja na nyumba tatu (3) za wafanyakazi. Uboreshaji wa miundombinu ya Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kilichopo Kigoma ulifanyika.
Maboresho hayo yanaenda sambamba na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa Mamlaka kupitia mafunzo mbalimbali ya muda mrefu na muda mfupi ndani na nje ya nchi.
Utekelezaji wa Mfumo wa Udhibiti wa Ubora wa Huduma
Mamlaka imeendelea kukidhi Viwango vya Ubora vya Kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga na hivyo anga la Tanzania kuendelea kuaminika kuwa salama. Katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ilifanyiwa ukaguzi wa kimataifa na Kampuni ya Certech ya Canada juu ya utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa ubora wa huduma “Quality Management Systems(QMS)” kwa mwaka 2021 na 2022 ambapo ukaguzi wa mwaka 2022 ulifanyika kuanzia tarehe 14 hadi 21 Januari 2023. Katika kaguzi hizo ubora wa huduma zinazotolewa na Mamlaka katika seekta ya usafiri na usalama wa anga zilionekana kukidhi mahitaji ya wadau, jambo ambalo liliwezesha Mamlaka kuendelea kushikilia cheti cha ubora wa huduma tajwa cha ISO 9001:2015.
Kielelezo 7: Cheti cha Ubora (ISO) kwa huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga ambacho Mamlaka ilipata baada ya ukaguzi wa mwaka 2022 uliofanyika kuanzia tarehe 14 hadi 21 Januari 2023.
Kuiwakilisha Nchi Kimataifa Katika Masuala ya Hali ya Hewa
TMA imefanikiwa kutekeleza vyema jukumu lake la kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa. Wataalamu mbalimbali wa Mamlaka wameendelea kutekeleza majukumu yao katika Vikosi kazi mbalimbali vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
TMA ilitekeleza vizuri dhamana ilizopewa kikanda na kimataifa na kufanikiwa kuitangaza vizuri TMA na Tanzania kimataifa. Wataalamu kumi na moja (11) wa TMA walioteuliwa kuhudumu katika vikosi kazi mbalimbali vya Kamisheni za WMO walishiriki vyema na kutoa mchango wa kitaalamu katika shughuli za vikosi kazi hivyo. Kutokana na ushiriki mzuri, TMA iliendelea kuaminiwa ambapo baadhi ya wataalamu walipewa majukumu ya uongozi. Dkt. Kabelwa ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya WMO ya Uchakataji wa Data na Utabiri wa Hali ya Hewa “Standing Committee on Data Processing for Applied Earth System Modelling and Prediction (SC-ESMP)”. Aidha, Dkt. Pascal Waniha, ambaye ni Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi katika Mamlaka aliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza wa kikosi kazi cha utekelezaji wa programu ya WMO “Task Team on Global Basic Observing Network (TT-GBON)”.
TMA ilishiriki vizuri katika kutoa mchango wa kitaalamu unaohusu sayansi ya hali ya hewa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi ambao ulichangia katika maamuzi yaliyotolewa kwa manufaa ya nchi yetu. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a alishiriki kwa mafanikio katika Mikutano ya Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na tabianchi, ikiwa ni pamoja na Mkutano wa 27 “Twenty-seventh session of the United Nations Framework Framework Convention on Climate Change Conference of the Parties (UNFCCC-COP-27)” uliofanyika Sharm El-Sheikh, Misri kuanzia tarehe 06 hadi 18 Novemba 2022. Katika Mkutano huo, Dkt. Ladislaus Chang’a aliongoza vikao vya Kamati ya Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabia nchi ya Ushauri katika masuala ya teknolojia “Subsidiary Body for Scientific and Technological Advice (SABSTA-57)” ambavyo vilikuwa ni sehemu ya majadiliano katika Mkutano wa COP-27. Ushiriki mzuri wa TMA uliwezesha Tanzania kuteuliwa kuwa miongoni mwa nchi zitakazonufaika na mpango wa WMO wa kuboresha uangazi wa hali ya hewa wa “Systematic Observation Funding Security (SOFF)”.
Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilikuwa mwenyeji wa kongamano la 15 la watumiaji kutoka Bara la Afrika wa data na huduma zitolewazo na Shirika la Satelati za hali ya hewa la Umoja wa Ulaya “The 15th EUMETSAT User Forum in Africa (15th EUFA)”. Kongamano hilo lilifanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania kuanzia tarehe 13 hadi 16 Septemba, 2022 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere “Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC)”. Kongamano hilo lilifanyika kwa mafanikio na kuitangaza TMA na Tanzania kimataifa katika nyanja mbalimbali kama vile vivutio vya utalii na Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa cha Kigoma. Pia ukarimu uliooneshwa kwa wageni kupitia huduma mbalimbali walizopewa na maeneo mbalimbali waliyotembelea yaliiletea sifa nzuri nchi yetu na kuchangia katika uchumi wa nchi kupitia huduma walizotumia washiriki wa mkutano. Hatua hiyo itachangia kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi za bara la Afrika na Bara la Ulaya.
Mashirikiano ya Tanzania na nchi mojamoja katika huduma za hali ya hewa kupitia Tume za Kudumu za Pamoja “Joint Permanent Commission (JPC) yaliimarika zaidi. Katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ilishiriki katika mikutano na mawasiliano mbalimbali yaliyohusisha JPC na nchi saba (7) ambazo ni Uganda, Msumbiji, Malawi, Afrika ya Kusini, Oman, Irani, na Rwanda.
Tafiti za kisayansi na ushirikiano na taasisi nyingine.
Mamlaka imeendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kufanya tafiti mbalimbali katika masuala ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ambapo katika kipindi cha miaaka miwili ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, jumla ya machapisho ya utafiti manne (4) yaliandaliwa na kuchapishwa katika majarida ya kimataifa ya sayansi. Wataalamu watano (5) kutoka Zanzibar walishiriki katika tafiti hizo. Tafiti hizi zimechangia katika kuboresha huduma zinanzotolewa na Mamlaka.
Aidha, Mamlaka imekuwa mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Masuala ya Usimamizi wa Ukanda wa Pwani na Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi kwa Zanzibar (Technical Committee of Integrated Coastal Zone Management issues and Climate Change matters for Zanzibar – ICZM) pamoja na kufanikiwa kuwa mjumbe kwenye kamati ya “Soil and Air Quality Technical Committee” ya Taasisi ya Viwango Zanzibar (Zanzibar Bureau of Standards- ZBS) na Kamati ya Tume ya Mipango Zanzibar ya kujadili mwenendo wa uchumi Zanzibar.
SHUKRANI NA HITIMISHO
Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yamepatikana kutokana na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita ya kuipatia Mamlaka vitendea kazi muhimu ikiwemo Rada na vifaa vya hali ya hewa kupitia bajeti ya maendeleo, kupatiwa fedha za kufanikisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa na pia kupatiwa wafanyakazi wapya.
Mafanikio haya yameifanya TMA kuweza kutimiza majukumu yake ya utoaji wa huduma, uratibu na udhibiti wa shughuli za hali ya hewa nchini kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 na pia kutimiza jukumu muhimu la kuiwakilisha Nchi kimataifa kwenye masuala ya hali ya hewa.
Aidha, Mamlaka inatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kufuatilia na kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa ajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa letu. Taarifa hizi za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ni rasmi, zimeboreshwa na zinakidhi viwango vya kimataifa.
Hali ya Hewa kwa Maendeleo Endelevu
No comments:
Post a Comment