SERIKALI imewataka wadau wa bandari kutumia vyema fursa za vikao vinavyofanyika mara moja kwa mwezi ili kuja na suluhu na mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji nchini katika Ziwa Viktoria.
Akizungumza katika kikao cha kwanza cha wadau wa maboresho ya bandari jijini Mwanza, Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mhandisi Aron Kisaka, amesema kukutana pamoja kutawawezesha wadau kuwasilisha taarifa za utendaji zinazoeleza mipango, mikakati na changamoto na namna ya kukabiliana na changamoto ili kuwa na uelewa wa pamoja.
“Napenda kuwashukuru kwa kushiriki katika kikao hiki na niwatake kuhakikisha yale yote tunayozungumza hapa tujiwekee na ukomo ili vikao vinavyofuata tujipime kama tunakwenda mbele au changamoto hizo ziende kwa mamlaka nyingine kwa maamuzi’ amesema Mhandisi Kisaka.
Mhandisi Kisaka amewataka wadau muhimu kama Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na Wamiliki wa Bandari zilizorasimishwa Mkoani Mwanza kutafuta masoko kwa nchi Jirani zinazotumia bandari za Kanda ya Ziwa ili kupata mzigo mwingi zaidi na kuinua pato la taasisi hizo na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa MSCL, Eric Hamis ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa meli lengo likiwa kuhakikisha kuna mazingira mazuri ya usafiri na usafirishaji katika Ziwa Viktoria.
Naye Meneja wa Bandari ya Mwanza Ferdinand Nyathi, amesema kupitia vikao hivi mipango mbalimbali ya wadau itawasilishwa kwa wadau ili kuwa na uelewa wa pamoja ambao matokeo yake itakuwa ni kuboresha miundombinu kwa utaratibu mzuri ambao tija yake itakuwa ni kuongeza pato la mamlaka, Taifa na mwananchi mmoja mmoja.
Meneja ameeleza mipango ya bandari ni kujenga gati maalum kwa bandari ya Mwanza, Kemondo na Kagera kwa ajili ya kuhudumia meli kubwa zaidi ikiwemo ya MV Mwanza hapa kazi tu ambayo inakamilishwa.
Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) inaendelea na mpango wake wa kusimamia vikao vya wadau wa maboresho ya bandari katika Bandari za Bahari ya Hindi, na kwenye Maziwa nchini lengo ni kuhakikisha bandari zinaleta ufanisi na tija na hatimaye kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji nchini.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
No comments:
Post a Comment