Kikosi cha timu ya majimaji enzi zake katika uwanja wa Majimaji mjini Songea kikiwa na wachezaji nyota kama vile Stephen Mapunda Galincha na wengine. |
MAJIMAJI ni miongoni mwa timu maarufu za soka hapa nchini ambayo ina historia ndefu ukiachia timu za Simba na Yanga ambazo zimedumu kwa muda wote zikicheza ligi kuu bara na kuwa na wapenzi lukuki kila kona ya nchi yetu.
Hakuna ubishi Timu ya Majimaji inafuatia kwa kuwa na washabiki na wapenzi wengi hapa Tanzania. Majimaji katika kipindi chake imepita katika vipindi vya mafanikio na changamoto.
Licha ya kupata mafanikio makubwa katika mchezo wa soko hapa nchini,Majimaji pia imekumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kushuka daraja mara kadhaa katika vipindi tofauti.
Historia inaonesha kuwa,Klabu ya Majimaji ilianzishwa mwaka 1977 na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma wa zamani na Katibu Mkuu Mstaafu CCM hayati Dkt. Rawrence Gama ambapo Kikosi cha kwanza cha Majimaji kiliweza kuundwa kwa kuichukua timu ya kombaini ya Mkoa wa Ruvuma na kupewa jina la Majimaji.
Kulingana na historia hiyo,Timu ya soka ya Majimaji ilipanda daraja na kucheza daraja la kwanza kwa wakati huo sasa ligi kuu, mwaka 1982 ambapo walicheza msimu mmoja na kushuka kutokana na wachezaji wake wakati huo hawakuwa na uwezo wa kuhimiri mikikimikiki ya ligi hiyo ambayo ilikuwa na timu nane kwa nchi nzima katika kipindi hicho.
Mwaka 1984 Majimaji ilirejea tena kucheza ligi hiyo kwa kasi baada ya kujipanga na kuwa moja ya timu ambayo ilikuwa na sifa ya kuwalipa fedha nyingi na maslahi bora wachezaji wake ,hali iliyosababisha baadhi ya wachezaji wa timu za Simba na Yanga kutoka Dar es salaam na kutimkia Songea kwa lengo la kujiunga na timu hiyo ya wanalizombe.
Wachezaji ambao walikuwa wakiwika kwa wakati huo kwa timu za Simba, Yanga na Pan African ambao walikuja kujiunga na timu hiyo yenye makao makuu yake mjini Songea, ni Peter Tino, Zamoyoni Mogela, Malota Soma na Inocenti Haule.
Hata hivyo mchezaji Innocent Haule baadaye aliamua kuachana na Majimaji na kutimkia nchini Kenya kucheza ligi za huko baada ya uongozi wa Simba kudai wachezaji hao walikuwa wamehama bila kufuata utaratibu wa uhamisho kutoka katika vilabu vyao.
Katika kipindi hicho Timu ya Majimaji ilikuwa tishio kwa vilabu vingine vilivyokuwa vikishiriki ligi hiyo na hata kusababisha kuchukua ubingwa wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa miaka miwili mfululizo mwaka 1985 na 1986 ambapo ligi hiyo ilikuwa ikishirikisha timu sita kati ya hizo timu tatu kutoka Visiwani na tatu kutoka Bara.
Majimaji katika mchezo wake wa kwanza wa mashindano ya klabu bingwa barani Afrika mwaka 1986 ilipangiwa na timu ya Dyanamo ya Zimbabwe, mchezo ambao ulifanyika mjini Harare makao makuu ya nchi ya Zimbabwe, katika mchezo huo Majimaji ilifungwa mabao 5-0.
katika mechi ya marudiano mchezo haukuweza kufanyika kwa sababu Timu ya Majimaji ilijitoa baada ya kupata ajali wakati ikitokea Songea kuelekea Dar es Salaam na baadhi ya wachezaji wake waliumia vibaya akiwemo Athumani Maulid na ikawa mwisho wake wa kucheza mpira.
Historia inaonesha kuwa,Mwaka wa pili Timu ya Majimaji ilipochukua ubingwa wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ilipangiwa mchezo wake wa kwanza kucheza na timu ya Shirika la Kilimo la nchi ya Madagasca(BTM) na kushinda bao 2-1.
Katika mchezo wake wa marudiano uliochezwa katika uwanja wa Taifa(Uhuru), jijini Dar es Salaam, Timu ya Majimaji ilishinda tena mabao 2-1 hivyo kusonga mbele, na kutolewa na FC Leopard ya Kenya kwa jumla ya mabao 2-0.
Timu ya Majimaji ilishuka daraja baada Muasisi wake,Hayati Dkt.Gama kuhama Mkoa wa Ruvuma na kuhamia Mkoa wa Tabora,hali ambayo ilisababisha timu hiyo kuanza kuyumba,baada ya viongozi wa Serikali ya Mkoa kushindwa kuchangia masuala ya michezo.
Hayati Dkt.Gama alipenda michezo na alikuwa mstari wa mbele kushughulikia changamoto zilizokuwa zinawakabili wachezaji.Hata hivyo Dkt. Gama akiwa Tabora aliweza kuusaidia Mkoa wa Tabora kuunda timu ya Mirambo iliyokuwa tishio katika ligi kuu Tanzania Bara.
Harakati ya Timu ya Majimaji kurudi tena kucheza ligi kuu Tanzania Bara, zilipata msukumo kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Songea mjini, Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye alihakikisha kuwa timu hiyo inarudisha heshima yake ya miaka ya nyuma ambapo alitoa hamasa kubwa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa soka mkoani Ruvuma na wale wanaoishi nje ya mkoa huo.
Timu ya Majimaji ilijiwekea mikakati iliyosababisha timu hiyo kupanda daraja na kucheza ligi kuu Tanzania Bara katika msimu wa mwaka 2009/2010 baada ya kucheza ligi ya daraja la kwanza Taifa na kufanikiwa kuwa kati ya timu tisa zilizoingia fainali ya kucheza ligi kuu.
Katika fainali hiyo timu tatu zilifanikiwa kuingia ligi kuu kufuatia kushika nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo,timu hizo ni Majimaji, Manyema na African Lyon.
Majimaji tangu ilipopanda daraja na kurudi ligi kuu Tanzania bara ilijitahidi kucheza.Hata hivyo kiwango cha Majimaji cha enzi zile bado hakijaonekana,hali ambayo imesababisha timu hiyo kupotea kwenye ulimwengu wa soka baada ya kushuka daraja kwa muda mrefu sasa.
Hata hivyo timu hiyo haina budi kuungwa mkono kwa hali na mali ili kuhakikisha kuwa wadau na wafadhili wanaichangia timu hiyo ili hatimaye kurejea ligi kuu na kurudisha heshima ya Majimaji ya enzi zile katika mchezo wa soka nchini.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
No comments:
Post a Comment