NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imefadhili ziara ya siku nne ya mafunzo kwa
Viongozi wa Vyama na Mashirikisho ya Wafanyabiashara Wadogo (Machinga) na
Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam, wanaoondoka nchini Jumatatu Februari
6, kwenda Kigali, Rwanda.
NMB imekabidhi tiketi 12 za kwenda na kurudi Rwanda kwa
wajasiriamali hao 10 na viongozi wawili, watakaoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya
Ilala, Edward Mpogoro na Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na Uzalishaji, Dk.
Elizabeth Mshote.
Makabidhiano hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es
Salaam, ambako Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa NMB, Benedicto Baragomwa, alimkabidhi
tiketi hizo Mkuu wa Mkoa, Mhe. Amos Makalla, ambaye ni mbunifu wa wazo la
kupeleka viongozi hao Kigali, kujifunza namna sahihi za kuendesha biashara zao
na Sekta ya Usafirishaji wa bodaboda.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuwaaga, RC Makala aliipongeza
NMB kwa kukubali kufadhili safari ya viongozi hao wa makundi hayo muhimu katika
mpango mkakati wake wa kuipandisha Dar es Salaam kutoka nafasi ya sita kwa
usafi barani Afrika, kuwa namba moja - inayoshikiliwa na Kigali hivi sasa.
"Nilipotembelea Rwanda, nikashawishika kutuma wawakilishi
wa kwenda kujifunza na nikawasilisha wazo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye
alilikubali na kulibariki. Bahati mbaya sikuwa na fungu la kufanikisha ziara
yao. Nashukuru NMB ikalipokea hili na kufanya uwezeshaji huu ambao unaunga
mkono jitihada za Serikali.
"Ni wazo lililokuwa linaunga mkono jitihada za Rais Samia
ambaye alikutana na Machinga Ikulu na kupanga nao mikakati ya kuboresha mazingira
ya utendaji kazi wao na kuleta tija kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Leo tunakabidhiwa tiketi na Jumatatu nitawasindikiza Uwanja wa Ndege mimi
mwenyewe," alisisitiza Makala.
Aliwataka viongozi hao kuitumia vema ziara hiyo kwa kuhakikisha
wanajifunza mbinu sahihi za uendeshaji shughuli katika mazingira yasiyokwaza
Mamlaka na Jamii, sanjari na kuwa mabalozi wema watakaovutia Wanyarwanda nao
kuja kujifunza katika maeneo mengine na kushirikiana nao kibiashara.
Kwa upande wake, Baragomwa alisema siri ya NMB kuitikia haraka
maombi ya kuwezesha ziara hiyo ni udau mkubwa ilionao kwa maendeleo ya jamii,
hivyo walilipokea ombi hilo kama jukumu lao la kuinyanyua kada hiyo ya Machinga
na Bodaboda kibiashara na kiuchumi.
Mbele ya Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard,
Baragomwa akasisitiza kuwa benki yake inajivunia ushirikiano baina yao,
Serikali na jamii, alioutaja kuwa umechangia faida kubwa ya Sh. Bilioni 429 kwa
mwaka 2022, pato lililotanua fungu la Program ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR)
kufikia Sh. Bilioni 6.2.
Alibainisha kuwa, kupitia ziara hiyo, viongozi hao watajifunza
mengi nchini Rwanda, ambako nao wametuma wawakilishi wawili, huku
akiwahakikishia huduma bora na rafiki pindi watakaporudi zikiwemo za NMB
MastaBoda na mikopo yenye riba nafuu kwa Machinga na wajasiriamali wadogo, wa
kati na wakubwa.
Aidha, DC Mpogoro alimshukuru RC Makala kwa wazo lake hilo
linaloenda kumaliza changamoto za kiutawala dhidi ya makundi hayo, huku
Mwenyeviti wa Machinga Dar, Namoto Yusuph na wa Bodaboda Dar, Saidi Chenja,
wakiiahidi NMB na Serikali kutumia ziara hiyo kwa ustawi wa shughuli zao na
miundombinu ya Jiji na usafi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment