ASKOFU, MHASHAMU RUWAICH AIPONGEZA JOLIFATZ - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 27 February 2023

ASKOFU, MHASHAMU RUWAICH AIPONGEZA JOLIFATZ

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu JUDE THADEUS RUWAICH, amesema dunia ipo kwenye zama za upekee ambazo zina maelekeo ambayo si rafiki kwa uhai.

Amesema hayo hivi karibuni ofisini kwake Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na wajumbe wanaounda Mtandao wa Waandishi wa Habari za Uhai na Familia – JOLIFATZ, walipoenda kuutambulisha Mtandao huo kwa Mhashamu RUWAICH.

Amefafanua kuwa kwa bahati mbaya bara la Afrika vionjo vya kutokuwa rafiki kwa uhai vinajipenyeza kwa kasi hivyo ni vyema kila mmoja atambue na kujipanga kukabiliana na changamoto hizo zisije kuota mizizi, na ili zisiote mizizi ni lazima kujua kuwa chimbuko ka uhai ni mwenyezi Mungu.

Askofu RUWAICH amebainisha kuwa mmiliki na mtoaji wa uhai ni mwenyezi MUNGU, kwa hiyo kama JOLIFA inajipanga kutetea, kulinda na kupalilia uhai itambue kwamba inafanya hili ikiwa inaienzi kazi ya Mungu.

“Ninyi mlio tayari kufanya hilo naomba muwe watangulizi wa wengi, muwaamshe wengi watambue kuwa uhai ni mali ya Mungu, ni zawadi ya Mungu na unapaswa kuheshimiwa na kutunzwa kwa namna ambayo inatufanya tumrudishie Mungu sifa na shukrani” 

Mtandao wa Waandishi wa Habari za Uhai na Familia – JOLIFATZ, unaoundwa na waandishi mbalimbali wa habari hapa nchini, wanaosukumwa kuutetea na kuulinda uhai, uliundwa rasmi mwishoni mwa mwaka jana ukijumuisha waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari. 

Malengo ya Mtandao huo ambao kwa sasa unajumuisha waandishi wa habari takribani ishirini na tano, ni kulinda thamani ya Uhai wa Binadamu kwa kupinga mitazamo na matendo yanayodhalilisha na kuharibu Utu wa binadamu, kubuni, kuandaa na kutekeleza Kampeni kwa ajili ya maendeleo ya kweli ya Binadamu kwa kuheshimu Tunu halisi za Utamaduni wa kiafrika.

No comments:

Post a Comment