VYAMA VYA SIASA RUKHSA KUFANYA MIKUTANO YA HADHARA - SAMIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 4 January 2023

VYAMA VYA SIASA RUKHSA KUFANYA MIKUTANO YA HADHARA - SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. George Simbachawene, Msajili wa Vyama vya Siasa Mhe. Jaji Francis Mutungi, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Mohammed Ally Ahmed pamoja na viongozi wa Vyama Vya Siasa mara baada ya Kikao Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 03 Januari, 2023.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametangaza maamuzi ya Serikali kuondoa zuio la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.

Aidha, Rais Samia amevitaka vyama vya siasa kuikosoa na kuishauri Serikali kupitia mikutano ya hadhara kistaarabu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo.

Rais Samia ametangaza maamuzi hayo wakati akizungumza na viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa 19 Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Serikali imedhamiria kuukwamua mchakato wa kupata Katiba mpya baada ya kukaa na kukubaliana na vyama vya siasa.

Vile vile, Rais Samia amesema hatua hiyo itazingatia hali halisi ya nchi, uwezo wa kiuchumi pamoja na mila na desturi zetu.

Wakati huo huo, Rais Samia amesema Serikali inajiandaa kurekebisha Sheria anuai zikiwemo Sheria za Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa ili kujenga taifa lenye umoja.

Rais Samia amesema ili taifa liwe moja lazima kuwe na maridhiano baina ya vyama vya siasa kwa lengo la kuendesha taifa lenye amani na utulivu kwa maendeleo ya taifa letu.

No comments:

Post a Comment