NGUVU ZA PAMOJA ZINAHITAJIKA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 22 December 2022

NGUVU ZA PAMOJA ZINAHITAJIKA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII


Na Faustine Gimu, Morogogoro

KATIKA kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuimarika ngazi ya Jamii, nguvu za pamoja zinahitajika ambapo wizara ya afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imekuwa mstari wa mbele kwa kuwa na mikakati mbalimbali ya uboreshaji wa huduma.

Hayo yamebainishwa mkoani Morogoro na Afisa Program huduma za afya ngazi ya jamii, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Orsolina Tolage katika kikao cha pamoja kilichoandaliwa na asasi ya kiraia ya SIKIKA kupitia mfuko wa dunia [Global Fund] chenye lengo la kujadili mafanikio, changamoto na kupeana uzoefu wa utekelezaji huduma za afya ngazi ya jamii katika afua za UKIMWI, Kifua kikuu [TB] na Malaria.

Tolage amesema ni muhimu kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii kwani ndio kiunganishi  kutoka kwenye jamii hadi katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Huduma za afya ngazi ya jamii ni kiunganishi muhimu sana hadi vituo vya kutolea huduma hivyo ni muhimu kuendelea kushirikiana na wadau tunakuwa kitu kimoja ili huduma za afya ziendelee kuimarika ndani ya jamii zetu,” amesema.

Ameendelea kufafanua kuwa kikao hicho kitaleta manufaa makubwa katika utekelezaji wa program ya afya ngazi ya jamii ikiwemo mikakati ya usafi wa mazingira .

“Sasa hivi kuna mambo mengi tunatakiwa tuangalie sio malaria, UKIMWI na TB peke yake kuna suala suala la usafi wa mazingira, magonjwa yasiyoambukiza, masuala ya lishe, masuala ya mama na mtoto, magonjwa ya mlipuko “amesema Tolage.

Aidha,Tolage ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za afya ngazi ya jamii kupitia Wizara ya Afya iliyo chini ya Waziri Mhe. Ummy Mwalimu .

Mkuu wa Programu ya Afya kutoka asasi ya kiraia ya SIKIKA Atu Mwangomale amesema kikao hicho kitakuwa na faida kubwa katika utekelezaji wa afya ngazi ya jamii huku mkurugenzi kutoka asasi ya kiraia ya HIMSO kutoka mkoani Mbeya Fadhili Mtanga akisema ni muhimu kufika huduma ya afya ngazi ya jamii bila kujali hali za uchumi.

Ikumbukwe kuwa asasi ya kiraia ya SIKIKA inatekeleza Huduma za afya ngazi ya jamii katika kwa afua za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria katika mikoa mitano ya Kigoma, Katavi, Geita, Simiyu na Ruvuma na halmashauri 14 zikiwemo Mpimbwe,Tanganyika, Mpanda TC, Uvinza, Buhigwe, Kigoma mji, Manispaa ya Songea, Tunduru, Mbinga, Chato, Geita, Mbogwe, Itilima na Bariadi ambapo kikao hicho kimekutanisha washiriki kutoka Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI, taasisi ya Benjamin Mkapa na asasi za kiraia [CSO,s]za MKUTA, BAKAIDS, PADI, ROA, SHDEPHA, EDOTA, UDESO na RUDIA.

No comments:

Post a Comment