SERIKALI imesema kukamilika kwa jengo la abiria linalojengwa katika kiwanja cha Ndege cha Arusha kunatarajiwa kupunguza changamoto kwa abiria wanaotumia kiwanja hicho na kuongeza pato la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa jengo la abiria litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 300 kwa wakati mmoja litakapokamilika linalojengwa na Kampuni ya Zhixin Construction Limited ambalo litagharimu takribani bilioni 2, Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupeleke Mwakibete, amesema utekelezaji wa maboresho ya kiwanja hicho unakwenda kwa awamu lengo ni kuhakikisha abiria wanapata huduma stahiki.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kufanya Filamu ya Royal Tour kwani matokeo yake ndio mnayaona hapa ndege zinashusha watalii kila wakati, hivyo Serikali lazima ihakikishe kiwanja kina miundombinu rafiki na kina uwezo wa kutoa huduma nzuri ili kuvutia abiria wengi zaidi” amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete amesema pamoja na maboresho hayo Serikali ina mpango wa kukiwekea taa kiwanja hicho ili kukiwezesha kuhudumia watalii na wasafiri wengine kwa saa 24.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Arusha Mhandisi Elipid Tesha, amesema maboresho yaliyoanza kufanywa kiwanjani hapo ni pamoja na barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, eneo la kuegesha magari ambapo kumeongeza miruko ya ndege kutoka 8,271 kwa mwaka 2020 mpaka 14,244 kwa mwaka 2022 huku likitajwa kuwa ni ongezeko la asilimia 41.
Mhandisi Tesha ameongeza kuwa pamoja na ongezeko la miruko kiwanjani hapo, pia mapato yameongezeka kutoka milioni zaidi ya 900 kwa mwaka 2021 mpaka kufikia bilioni moja nukta 2 mwaka 2022 hivyo kukifanya kiwanja hicho kuvuka lengo la ukusanyaji.
Naibu Waziri yuko Mkoani Arusha kukagua miradi na kutembelea taasisi kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na sekta ya Uchukuzi.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)

No comments:
Post a Comment