![]() |
| Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo akiwasilisha mada kuhusu fursa za biashara na uwekezaji katika kanda ya Afrika katika mkutano wa mabalozi unaoendelea Zanzibar. |
MABALOZI wa Tanzania katika kikao chao cha kutathimini utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kinachofanyika mjini Zanzibar tarehe 14 hadi 21 Novemba 2022 pamoja na mambo mengine, walieleza kuwa Bara la Afrika lina fursa nyingi na kinachotakiwa ni bara hilo kujipanga ili liweze kunufaika na fursa hizo.
Akiwasilisha mada kuhusu fursa za bara hilo, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Mhe. Innocent Shiyo alisema kuwa asilimia 60 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani inapatikana barani Afrika na endapo itatumika vizuri ina uwezo wa kulisha dunia nzima kwa asilimia 60, hivyo ni muda muafaka kujipanga ili kutumia fursa hiyo kujiendeleza kiuchumi.
Alitoa mfano kuwa Bara la Afrika kwa mwaka linaagiza chakula chenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 40.5 kutoka nchi mbalimbali. Hizo ni fedha nyingi ambazo zingeweza kuokolewa na kunufuisha bara la Afrika, endapo ardhi iliyopo ingetumika ipasavyo.
Katika mada hiyo ambayo iliibua masula mengi ya kuyajadili, iliainisha pia kuwa Bara la Afrika linakidhi asilimia 30 ya madini yote duniani, asilimia 8 ya gesi yote duniani, asilimia 40 ya dhahabu yote duniani, asilimia 100 ya tanzanite yote duniani na asilimia 90 ya madini ya chromium na platinum. Hizo ni fursa nyingi ambazo hazijatumika vizuri ili kulinufaisha bara hilo.
Kutokana na fursa hizo lukuki barani Afrika, Balozi Shiyo alibainisha kuwa Dunia inalitazama Bara la Afrika kama eneo la kimkakati la ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili dunia kama za usalama wa chakula, nishati, malighafi za viwandani, masoko ya bidhaa mbalimbali na masuala ya kimazingira. Hivyo, ni jukumu la Afrika kuweka mikakati ya kujikwamua ili liweze kunufaika na mahitaji ya dunia.
Kwa upande wa Tanzania, imeelezwa kuwa nchi hiyo ina fursa nyingi ikiwa ni pamoja na eneo zuri la kijiografia la kupakana na nchi nane ambazo kati ya hizo sita hazina bandari. Imeelezwa kuwa kupitia bandari zake, Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika vyema kiuchumi endapo itafanikiwa kuzishawishi nchi hizo sita kutumia bandari za Tanzania.
Mabalozi wa Tanzania wanaendelea na kikao chao cha wiki moja mjini Zanzibar kilichoanza tarehe 14 Novemba 2022 kinacholenga kuweka mkakati mpya wa utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi. Kwa siku ya leo tarehe 15 Novemba, 2022 Mabalozi pamoja na wakuu wa taasisi za umma na binafsi wanajadiliana namna watakavyoweza kushirikiana kutatua changamoto ambazo kwa namna Moja au nyingine zinakwamisha utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali


No comments:
Post a Comment