Na Munir Shemweta, WANMM MBARALI
SERIKALI imeamuru vijiji vitano na vitongoji 41 katika vijiji 14 pamoja na sehemu ndogo ya kitongoji cha magwalisi kilichopo mamlaka ya mji mdogo wa Rujewa wilaya ya mbarali kuhamishwa ili kupisha hifadhi. Pia vitongoji 3 katika kijiji cha Lualaje wilayani Chunya navyo vinatakiwa kuondoka kupisha hifadhi.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 25, 2022 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula katika mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo la Ubaruku Mbarali wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta walipofanya ziara kwenye eneo la mto ruaha na mnazi katika kijiji cha Mwanavala ambapo eneo lote liko katika hifadhi.
Uamuzi huo wa serikali unalenga kutunza na kulinda ardhi oevu pamoja na vyanzo vya kupokea na kutunza maji yanayotiririka kutoka mito mbalimbali. Alivitaja vijiji vitakavyoondoka kwa asilimia mia moja kuwa ni Luhanga, Madundasi, Msanga, Iyala na kalambo vyenye idadi ya watu 21,252 na kusisitiza watu wa maeneo hayo wanatakiwa wasiwepo na usajili wa vijiji hivyo kufutwa.
‘’Katika zoezi hili wenye kulipwa fidia watalipwa na wale wasiostahili wataondoka kama walivyokuja na lengo la serikali ni kuwa na urithi wa watu wote’’ alisema Dkt Mabula.
Adha, Dkt Mabula alisema serikali imeridhia vijiji 15 vyenye ukubwa wa hekta 74, 324.12 na ranchi ya Usangu ya NARCO kuendelea kubaki huku vijiji vyote vinavyopakana na hifadhi ya Ruaha kufanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi.
Katika mapendekezo yake timu ya wataalamu ilipendekeza eneo la ranchi ya usangu linalopendekezwa kuondolewa ndani ya hifadhi litumiwe na wafugaji watakaohamishwa kutoka kwenye vijiji na vitongoji vinavyopisha hifadhi.
Aidha, Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya za Mbarali na Chunya pamoja na wadau wengine waandae mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vyote vinavyopatikana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Pia Ofisi Tamisemi iwe inashirikiana wadau wote muhimu katika suala la usajili wa vijiji na vitongoji ili kuepusha migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza miongoni mwa wadau ni wizara ya ardhi, wizara ya maji, maliasili na utalii, ofisi ya makamu wa rais mazingira.
Uhifadhi wa Bonde la Usangu ulianza mwaka 1953 wakati eneo likijulikana kama pori tengefu la utengule likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 500 kwa lengo la kuhifadhi bioanuwai katika ardhi oevu ya ihefu.
kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira na vyanzo vya maji uliofanyika miaka ya 1990 serikali iliamua kupandisha hadhi pori tengefu la utengule na kuwa Pori la Akiba la Usangu likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 4148 kwa tangazo la serikali namba 436A la tarehe 24 julai 1998.
Hata hivyo, uharibifu ulisababisha serikali kuja na mkakati wa kitaifa wa hifadhi ya mazingira ya ardhi oevu na vyanzo vya maji mwaka 2006 na kutaka bonde la usangu kuwa kati ya maeneo ambayo wafugaji waliovamia mabonde na maeneo ya vyanzo vya maji waondolewe.
Bonde la usangu ni ardhi oevu ya usangu ni kitovu cha kupokea na kutunza maji yanayotiririka kutoka mito mbalimbali ikiwemo mto Mkoji , Chimala, Kimani, Mbarari , Ndembera na Mzombe inayoanzia katika wilaya ya Wanging'ombe , Makete, Mufindi, Mbeya vijijini na Chunya na kuchangia maji kwenye mto Ruaha. Pia ni makazi ya bioanuwai mbalimbali ikiwemo wanyamapori, ndege wakubwa kwa wadogo aina zaidi ya 300 , samaki na mimea ya aina mbalimbali.
No comments:
Post a Comment