SERIKALI YATOA BILIONI 3 KUJENGA SEKONDARI YA WASICHANA MKOA RUVUMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 2 September 2022

SERIKALI YATOA BILIONI 3 KUJENGA SEKONDARI YA WASICHANA MKOA RUVUMA

 

 Baadhi ya vyumba vya madarasa katika Sekondari ya wasichana  ya Mkoa wa Ruvuma ambayo inajengwa eneo la Migelegele wilayani Namtumbo.

SERIKALI imetoa shilingi bilioni tatu kutekeleza mradi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma ambayo inajengwa katika eneo la Migelegele wilayani Namtumbo.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa mradi wa sekondari hiyo ambayo inatarajia kuanza kuchukua wanafunzi  mwakani.

Kanali Laban amesema Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa kumi ambayo serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari za wasichana za mikoa.

“Mheshimiwa Rais anatafuta fedha kuhakikisha miradi mbalimbali inatekelezwa ukiwemo mradi huu wa sekondari ya wasichana, nawapongeza wote  kwa kujitoa kusimamia kuhakikisha mradi huu unakamilika’’, alisisitiza Kanali Thomas.

Hata hivyo amesema kuna baadhi ya mikoa inayotekeleza mradi huu, hawajafikia hatua hiyo, amewaomba kutobweteka badala yake kuhakikisha ujenzi unakabilika ndani ya mkataba.

Ametoa rai kwa wataaalam wanaosimamia mradi huo kufanya kazi  kwa uaminifu, weledi na kufuata sheria  na kanuni, amewatahadharisha kuacha tabia ya udokozi wa pesa za miradi hali ambayo inaweza kusababisha kuchukuliwa hatua na kuanza kulaumu.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt.Julius Ningo ameahidi kusimamia kikamilifu mradi huo ili uweze kukamilika kwa viwango na ubora unaolingana na fedha zilizotumika.

Naye Afisa Elimu Halmashauri ya Namtumbo Juma Fulluge amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa  kupeleka fedha nyingi za ujenzi shule ya wasichana ya Mkoa wa Ruvuma.

Amesema katika awamu ya kwanza zaidi ya shilingi bilioni 1.6 zimetolewa ambazo zimejenga madarasa vyumba 12, mabweni Matano, maabara tatu, vyoo na nyumba za walimu.

Hata hivyo amesema ujenzi ambao unaendelea hivi sasa ni  jengo la utawala na ukumbi wa shule ambapo amesema shule hiyo itakapokamilika kwa asilimia 100 itakuwa ni miongoni mwa shule bora mkoani Ruvuma.

No comments:

Post a Comment