MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli 2022 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, huku ukibainisha kwamba maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani. TMA imesema mvua hizo pia zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa, huku zikiwa na mtawanyiko usioridhisha na kuambatana na vipindi virefu vya ukavu.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Makao Makuu ya TMA, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dk. Agnes Kijazi amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2022 ukanda wa Ziwa Victoria, huku kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini zikitarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya mwezi Oktoba na wiki ya kwanza ya mwezi Novemba.
"...Vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu wa vuli hususani maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki. Upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi," alisema Dk. Kijazi.
Aliongeza kuwa upungufu wa maji safi na salama unaweza kujitokeza na kuweza kuchochea magonjwa ya mlipuko, na Upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hivyo kupelekea migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Hata hivyo alibainisha kuwa kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua hivyo kunaweza kupelekea upungufu wa maji kwa matumizi mbalimbali.
Aidha aliitaka mikoa itakayo kuwa na mvua za chini ya Wastani hadi Wastani kuwa ni pamoja na Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma hasa wilaya za Kibondo na Kakonko na maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa Victoria.
"...Katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Simiyu mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2022. Mvua zinatarajiwa kuisha mwezi Januari, 2023. Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba): Mvua zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini." alifafanua Dk. Kijazi.
Alisema kwa Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki katika Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mvua zinatarajiwa kuwa za Chini ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi ya Nyanda za juu Kaskazini Mashariki. Mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya mwezi Oktoba na wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2022 na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu, mtawanyiko na mwendelezo usioridhisha katika maeneo mengi.
Akitaja baadhi ya athari alisema upungufu wa unyevunyevu wa udongo unatarajiwa kuathiri shughuli za kilimo, huku upungufu wa mvua ikitarajiwa kuathiri upatikanaji wa maji na malisho kwa ajili ya mifugo na upatikanaji wa chakula kwa ajili ya samaki, hali pia itakayo athiri uzalishaji wa mifugo pamoja na mazao yake.
"...Wadau wa sekta za mifugo na uvuvi wanashauriwa kuweka mipango madhubuti ya matumizi sahihi na uhifadhi wa maji na malisho ya mifugo. Aidha, wafugaji na wavuvi wanashauriwa kufuatilia na kutumia taarifa sahihi za utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani katika maeneo yao," alishauri Dk. Kijazi ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa WMO.
Katika sekta ya afya upungufu wa upatikanaji wa maji safi na salama inaweza kujitokeza na hivyo kusababisha magojwa ya mlipuko katika maeneo husika kama vile vikope, magonjwa ya ngozi, kipindupindu na homa ya matumbo. Wizara za kisekta na taasisi mbalimbali zinashauriwa kuchukua hatua mahususi kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.
No comments:
Post a Comment