SERIKALI YAIPA KONGOLE MULTICHOICE KUTANGAZA KOMBE LA DUNIA KWA KISWAHILI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 3 September 2022

SERIKALI YAIPA KONGOLE MULTICHOICE KUTANGAZA KOMBE LA DUNIA KWA KISWAHILI

Wadau wa sekta ya Sanaa na Michezo wakiwa kwenye hafla ya Maonesho kwa Vyombo vya Habari ya iliyoandaliwa na Kampuni ya Multichoice kupitia DStv Septemba 01, 2022 jijini Dar es Salaam.

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imeipongeza Kampuni ya Multichoice kupitia DStv kuamua kutangaza kwa Kiswahili Mashindano ya Kombe la Dunia yanayotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu nchini Qatar.

Akizungumza Septemba 01, 2022 Dar es Salaam katika hafla ya Maonesho Kwa Vyombo vya Habari ya Kampuni hiyo, kwa Niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Mohamed Mchengerwa, Naibu Katibu Mkuu Saidi Yakubu ameipongeza DStv kwa kuendelea kuunga mkono maendeleo ya Sekta ya Sanaa na Michezo nchini. 

“Nitumie nafasi hii kuwapongeza DStv,  kwa kutambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili na kuamua kutangaza mechi 64  za  Kombe la Dunia la FIFA mwaka 2022 kwa lugha hiyo, ili Watanzania wengi waburidike kupitia lugha yao" amesema Ndugu Saidi Yakubu.

Amesema DStv imeendelea kuonesha Dunia maudhui ya kitanzania kupitia filamu zinazooneshwa Chanel ya Maisha magic Bongo na Maisha Magic Poa ambayo imesaidia watanzania kuonesha vipaji na kupata kipato.

Ameongeza kuwa, Kampuni hiyo imekua Mdau mkubwa wa wizara katika hasa katika kipindi hichi ambacho sekta zake zimekua na ubunifu ambao umeleta tija kwa taifa.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Yakubu, ameishukuru kampuni hiyo, kwa kuanzisha programu za kusaka vipaji katika tasnia ya filamu, sambamba na kutoa ajira kwa watanzania.

Amesema kuwa, soko la filamu za kitanzania limepanuka na limeingia katika ushindani wa Kimataifa, ikiwemo katika Tuzo za Africa Magic Viewers Choice Awards, ZIKOMO na Zanzibar International Film Festival.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa, changamoto ya Hakimiliki katika kazi za ubunifu imeendelea kufanyiwa kazi, ambapo hivi karibuni Mhe.Waziri aliunda Kamati ya kushughulikia kero hiyo ambayo tayari imewasilisha mapendekezo na Serikali inayafanyia kazi.

Shughuli hiyo imehudhuriwa pia na Balozi wa Afrika Kusini nchini Noluthando Malepe na Balozi wa Qatar nchini Khalifa Al Homaid.


No comments:

Post a Comment