DKT. AGNES KIJAZI AKABIDHIWA UFUNGUO WA JIJI LA ENTERPRISE, ALABAMA-MAREKANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 30 July 2022

DKT. AGNES KIJAZI AKABIDHIWA UFUNGUO WA JIJI LA ENTERPRISE, ALABAMA-MAREKANI


Enterprise, Alabama, Marekani

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt Agnes Kijazi, amekabidhiwa ufunguo wa Jiji la Enterprise, Alabama-Marekani na Mstahiki Meya wa Jiji hilo Bw. William E. Cooper alipowatembelea wataalamu kutoka TMA na mjumbe kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi) wanaoshiriki katika zoezi la kuhakiki utendaji kazi wa radar za hali ya hewa (“Factory Acceptance Test (FAT)”) katika kiwanda cha Enterprise Electronics Corporation-EEC kilichopo katika Jiji la Enterprise, kuanzia tarehe 18 hadi 29 Julai, 2022.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mstahiki Meya Cooper alisema amefurahishwa na ushirikiano uliopo kati ya EEC na TMA katika eneo la ununuzi na matengenezo ya Rada za Hali ya Hewa, na kuwakaribisha katika mji wa Enterprise. Kwa heshima ya ushirikiano huo, Mstahiki Meya alimkabidhi Dkt Kijazi Ufunguo wa Jiji la Enterprise ikiwa ni heshima ya pekee kuwa anakaribishwa katika Jiji la Enterprise.

“Nakukabidhi ufunguo huu kama alama ya heshima unayopewa katika jiji la Enterprise kwamba unaweza kuingia na kutoka upendavyo, aidha, umjulishe Balozi wa Marekani nchini Tanzania kuhusu wewe kupatiwa ufunguo huu”. Alisema Bw. Cooper.

Aidha, Mstahiki Meya pia alimpatia zawadi ya sanamu ya kumbukumbu ya historia ya Jiji la Enterprise yenye kuelezea namna mdudu mharibifu wa zao la pamba (boll weevil) alivyobadilisha shughuli za kilimo za eneo la Enterprise kutoka kilimo cha zao la pamba miaka ya 1800 hadi 1900 na kugeukia kilimo cha zao la karanga ambalo limekuwa na manufaa makubwa katika uchumi wa jiji la Enterprise.

“Mabadiliko hayo yamefanya mdudu huyu aheshimiwe kwamba kupitia uharibifu wake amesababisha mageuzi yenye mafanikio katika sekta ya kilimo.Ukipita katika baadhi ya maeneo ya jiji hili la Enterprise utaona sanamu hii ambayo ina historia muhimu katika mageuzi ya kilimo katika jiji hili”. Alieleza Bw. Cooper.

Kwa taarifa zaidi tembelea: www.meteo.go.tz

No comments:

Post a Comment