MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kuwa Serikali imedhamiria kuzitafutia ufumbuzi changamoto za elimu hapa Visiwani, ili kuleta mageuzi na kuirejesha hadhi ya sekta hiyo kimataifa.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Juni 2,2022 kisiwani Pemba katika mwendelezo wa Ziara zake za Kutembelea Taasisi mbalimbali za Elimu Zanzibar.
Amesema kuwa kihistoria, hadhi ya elimu Zanzibar kimataifa ilikuwa ni kubwa na ya kujivunia, ingawa katika kipindi cha kati ilikabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni wajibu kushikamana kwa hali na mali ili kuzitatua.
Mhe. Othman amekariri changamoto hizo kama zilivyobainishwa na wadau mbali mbali wakiwemo walimu, wakufunzi na wanafunzi, zikiwemo za ukosefu wa mipango na sera makini, uhaba wa vitendea-kazi, maslahi na udhaifu wa miundombinu, ambazo amesema hapana budi kuzikabili ili kufikia maendeleo ya kweli, kupitia hadhi ya elimu.
Akikhitimisha ziara yake hiyo iliyoanza Machi mwaka huu kisiwani Unguja, pamoja na kupata fursa ya kubadilishana mawazo na Walimu Wakuu wa Kisiwani Pemba katika Ukumbi wa Skuli ya Fidel Castro, Mheshimiwa Othman amewahimiza wahusika wote wa Sekta ya Elimu kuzidisha juhudi, ubunifu, moyo wa kujitolea na ujasiri, ili kuisogeza Zanzibar katika mstari wa mbele wa maendeleo duniani, na ili hatimaye kuyaepuka maisha ya usindikizaji.
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Leila Mohamed Mussa, amesema kuwa mageuzi katika sekta hiyo hayawezi kuepukika, na licha ya changamoto nyingi zilizopo, faraja ya kuyafikia malengo ya kuikwamua inakuja, hasa pale ambapo Viongozi wakuu, akiwemo Rais Dokta Hussein Ali Mwinyi na Wasaidizi wake, wakionekana kupania katika kuleta maendeleo ya kweli katika elimu, hapa nchini.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Othman ametembelea taasisi mbali mbali za elimu zikiwemo Chuo cha Kiislamu cha Kiuyu Micheweni, Skuli ya Kiislamu ya Ambasha na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Benjamin William Mkapa, zote za Kisiwani Pemba.
Viingozi mbali mbali wamejumuika katika Ziara hiyo, wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Maafisa Wadhamini, Vyama vya Siasa, Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Wakurugenzi na Watendaji kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.
No comments:
Post a Comment