WASAFIRISHAJI WAMPONGEZA RAIS SAMIA, WAOMBA SUBIRA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 11 May 2022

WASAFIRISHAJI WAMPONGEZA RAIS SAMIA, WAOMBA SUBIRA

 

CHAMA cha Wasafirishaji Tanzania (TAT-Tanzania Association of Transporters) kimempongeza Rais Samia Hassan na Serikali kwa hatua inazochukua kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha kunakotokana na wimbi la kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

TAT chenye wanachama wasafirishaji wa mizigo na mafuta zaidi ya 200, na ambacho ndicho chama kikubwa nchini, kimekuwa kikifuatilia kwa karibu mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta nchini na changamoto zake kwa kuwa athari zake zinakigusa moja kwa moja kutokana na kwamba magari ya wanachama wake husafirisha kila siku bidhaa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Msemaji wa TAT Omar Kiponza, amesema pamoja na changamoto zote zinazowakabili  Watanzania na Sekta ya Usafirishaji, TAT kinaamini kwamba ufumbuzi wa matatizo hayo utapatikana kwa kutumia busara na hekima inayoonyeshwa na Rais Samia na Serikali nzima.

“Pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta, katika siku za karibuni yamekuwapo matukio ya migomo ya madereva na sintofahamu kadhaa ndani ya Sekta ya Usafirishaji, TAT kinaamini kwamba yote hayo yatatatuliwa kwa kuyakabili kama Watanzania tunaopenda na kuitakia mema nchi yetu,” alisema Kiponza.

Rais wa TAT Mohamed Abdullah, alisema kwamba ni kweli wapo wasafirishaji wachache wenye changamoto na pia kuna baadhi ya madereva ambao nao wana matatizo, lakini yote haya yanaweza kumalizwa kwa kukumbuka kwamba sisi ni Watanzania, na rabsha katika Sekta ya Usafirishaji zinaipaka matope nchi, Serikali na Watanzania wote.

“Serikali inaendelea kushughulikia suala la bei za mafuta na haya mambo ya migomo ya madereva na kero za baadhi ya wasafirishaji. Tuipe muda na tuwe na subira. Tunampongeza Mama Samia na  Serikali kwa hatua inazochukua.

“Unaweza kusema haya yanayotokea sasa ukiacha mafuta kupanda, ni mambo yasiyo ya afya kwa Sekta ya Usafirishaji na kwa nchi yetu. Kuna baadhi ya madereva wanatumiwa. Nia ni kudhoofisha Bandari ya Dar es Salaam, Sekta ya Usafirishaji  na uchumi wa nchi yetu.

“Madereva ni ndugu zetu, kama kuna stahili zao wapewe. Wasafirishaji wanaopindisha haki waache mara moja na sote kwa pamoja tujihadhari na chokochoko za kutoka nje ya nchi zenye malengo ya kutufanya tugombane wenyewe kwa wenyewe kwa faida ya watu na biashara za nje,” alisema Mohamed Abdullah.

Wiki hii (Jumanne, Mei 10, 2022) Serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati January Makamba, ilitangaza hatua kadhaa za kukabili kupanda kwa bei za mafuta zikiwamo ruzuku ya shilingi bilioni 100 na ruksa kwa wafanyabiashara wenye mitaji kuingiza mafuta.


No comments:

Post a Comment