Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge ameongoza uzinduzi wa kampeni ya siku nne ya chanjo ya matone ya polio kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
Kampeni hiyo ya siku nne ambayo imezinduliwa kimkoa Kata ya Iguguno wilayani Mkalama imeanza leo Mei 18 ambapo itamalizika Mei 21 mwaka huu.
Akizungumza wakati akizindua kampeni hiyo Mahenge alianza kwa kuelezea kazi kubwa iliyofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga bajeti kubwa kwa upande wa sekta ya afya ambapo kwa Mkoa wa Singida pekee kwa mwaka huu walipokea zaidi ya Sh.30 Bilioni huku hospitali za wilaya zikijengwa Ikungi, Manyoni, Mkalama na Singida DC kwa wakati mmoja na ndani ya mwaka mmoja.
Mahenge aliongeza kuwa katika mkoa huo katika sekta ya afya vinajengwa vituo vya afya 15 katika wilaya zote huku Iramba ikiwa na vituo vitano na kueleza kuwa hiyo sio kazi ndogo bali ni kazi kubwa anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan.
"Nimetangulia kuyasema haya ili kuonesha jinsi Rais wetu Samia Suluhu Hassan anavyo tujali watanzania na ndio maana leo tupo hapa tunazindua kampeni hii ya polio baada ya Serikali kutuwezesha" alisema Dk.Mahenge.
Alisema kazi kubwa ya serikali si kuangalia mienendo ya nchi pekee bali na ya nchi za jirani na ndio maana baada ya kugundua nchi ya Malawi kuna kirusi cha polia ndipo juhudi zilipoanza kuchukuliwa kwa kutoa kinga ya polia katika baadhi ya mikoa inayopakana na nchi hiyo lakini ili tuwe na uhakika serikali imeagiza chanjo hiyo ifanyike mikoa yote.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick alisema kwa mkoa huo wanatarajia kuwafikia watoto waliochini ya miaka mitano 286,736 na kuwa maandalizi yote yamekamilika.
Dk.Ludovick alisema chanjo hiyo itatolewa kwa siku tatu na lengo ni kufika kwenye maeneo yote na kuwa itafanyika nyumba kwa nyumba .
"Madhara ya ugonjwa wa Polio ni ulemavu wa ghafla wa viungo na usiotibika kwa hiyo ni muhimu sana kwa kila mzazi na mlezi wawatoe watoto wao wenye umri tajwa wapate chanjo hii ambayo ni salama" alisema.
Dk. Ritha Willilo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) aliwaomba wazazi kutoa ushirikiano wa kuwatoa watoto wao ili kupata chanjo hiyo na kusema kauli mbiu isemayo tone moja la chanjo ya polio linatosha kabisa kuwakinga watoto wetu dhidi ya ugonjwa wa kupooza wa polio.
Diwani wa Viti Maalumu (CCM) Kata ya Iguguno Mariam Hussein akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kata hiyo alishukuru Serikali kusogeza huduma hiyo ya chanjo hadi walipo wananchi hivyo itaweza itaweza kuwafikia watoto wengi.
Kampeni hii inafanyika nchi nzima baada ya Serikali ya Malawi kutoa tamko mapema mwaka huu la kuwepo mlipuko wa Polio katika nchi hiyo baada mtoto mmoja kudhibitika kuwa na Polio na hivyo kuwa ni mara ya kwanza kwa bara ya Afrika kutokea changamoto hiyo baada ya kupita miaka mitano pasipo kuwepo na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment