UTANI WA KABILA LA WAHAYA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 3 December 2021

UTANI WA KABILA LA WAHAYA


ADELADIUS MAKWEGA, MBAGALA

HILI kuufahamu utani kwa kabila la Wahaya, ni vizuri mtu kwanza kufahamu mahusiano ya kabila hili katika familia zao yenyewe yakoje? Vizazi katika kabila hilo vina mahusiano kutoka kizazi cha kwanza hadi kizazi cha nne, yaani babu, baba, mjukuuu (mtoto) na kitukuu. Kwa utaratibu wa kimaisha tangu enzi uhai wa binadamu umekuwa ukiagukia katika vizazi hivyo vinne tu kuonana na nadra sana kuweza kuwepo kwa kizazi cha tano au sita  ambacho ni kining’inila ama zaidi ya hapo. 

Kining’inila huwa ni nadra sana kuonana na vizazi vya awali labda tu kwa simulizi tu.

”Baba wa babu yetu alikuwa mrefu mweusi na alikuwa anapenda sana kuwinda.”

Kwa wahaya mjukuu wa kiume anamuita bibi yake mzaa baba/mama mukaziwa/mugore yaani mkewe. Naye bibi huyu anamuita mjukuu wake mwami yaani mumewe.

Mjukuu huyu wa kiume anaweza akamuuliza bibi yake kuwa chakula kipo wapi? na bibi atajibu kuwa unadai chakula mbona haujaleta kuni/mboga. Ukiyatazama majibu ya bibi anayojibu kwa mjukuu, mbona hajaleta vitu vidogo vidogo yaani kuni na mboga. Bibi huyu hawezi sema haujaleta unga/ mchele au ndizi. Majibu haya yana maana kubwa sana kwa jamii hii. Hapo ndani yake kuna utani ambao mara zote huambatana na tabasamu na vicheko na wakati mwingine hata hasira za kuigiza.

Mjukuu akienda kwa bibi yake hata kama anakaa jirani anapokelewa kana kwamba ametoka mbali kama mgeni wa mbali lakini yote hiyo ni heshima ya utani kwake. Bibi atasema Ija mwami, Ija nyongela akimaanisha karibu mume wangu jisikie upo nyumbani. Akifika hapo mjukuu atapatiwa kahawa ya kutafuna huku bibi akisema kuwa naona kama ninapoteza zawadi zangu nazokupatia bure leo hii, siku hizi haunipendi. Kwa kuwa unaniacha mwenyewe tu.

Wahaya hawana utani baina ya baba na watoto wake labda nadra sana. Watoto wanapaswa kuwaheshimu mno wazazi wao. Utani unaweza kuonekana kwa baba/mama anapomtembelea mwanawe aliyepata mtoto (mjukuu) hapo baba/mama (babu) utamsikia akisema mukazina wangwe akimuita huyu mjukuu ni mke wangu. Kabila hili lina utani baina yake na makabila mengine kwa kuwa wanaishi jirani na Wajaluo kando ya Ziwa Victoria.

Wanautani baina yao na familia zilizooleana huku utani baina ya wifi na wifiwe, babu na mke wa mjukuu wake. Kwa mfano mjukuu akienda kwa babu yake na mkewe. Babu atasema kuwa ahh umemleta mke wangu. Mjuku anaweza akamjibu unamtaka? Kama unamtaka ngoja kwanza nimchoke, nitakuletea.

Babu anaweza kusema sawa ngoja ukimshindwa kumtunza mimi nitakusaidia kumtunza maana nyie vijana hamuwezi kutunza wake zenu. Babu anaweza kusema sawa na usipomleta tena hapa sintokuruhusu kuingia nyumbani kwangu. Mjukuu anaweza kusema kuwa nitakuja na nitaingia tena kama nilivyokuja leo nikiwa na mke mwingine.

Kaka wa bwana harusi / kaka wa bibi harusi, dada wa bwana harusi / dada wa bibi harusi huwa hawana utani kabisa hawa ni watu wanaoheshimiana mno. 

Kuna sherehe inaitwa Kishaija Nyabaki hii ni sherehe ya harusi ambayo hufanyika siku tatu kabla ya harusi, ukoo wa bwana harusi hufunga safari hadi kwa bibi harusi huku kukiwa na kundi kubwa la watu nyuma yao. Katika shughuli hiyo kuna mabinti hupiga ngoma na kucheza mbele ya wageni. Wageni wa ukoo wa bwana harusi hubeba mitungi mitatu hadi sita ya pombe za asili na wakifika hapo hupokelewa.

Jamaa hawa wakifika watapokelewa watasema neno kuwa wamekuja kumchukua bibi harusi, wakishasema neno hilo ule upande wa bibi harusi tangu babu/bibi, baba/ mama dada/kaka wote wanatoka ndani. Hapa babu wa bibi harusi atasimama na kusema ehh kulikoni mmekuja kumchukua mke wangu?

Hapa baba wa bwana harusi anajibu kuwa ni kweli kwa kuma wewe umeshindwa kumtunza. Hapa babu wa bibi harusi atajibu mnasemaje? Huyu nimemlipa posa, nina pombe nzuri kuliko hizi zenu, wewe baba gani? Hapa hapa baba wa bwana harusi atawaambia sasa mnasemaje?

Babu wa bibi harusi atasema kwanza nionesheni huyo anayetaka kumchukua mke wangu hili nimfundishe adabu. Baba wa bwana harusi atajibu yupo mwanaume tena wa shoka. Hapa babu wa bibi harusi atasema kuwa ah ah huyu ni mke wangu na nimefunga naye ndoa miaka mingi sana je utakubali kuoa mke ambaye tayari ameshaishi na mimi? Nawaombeni ondokeni na hata huyo mke wa kuoa hayupo hapa.

Katika lile kundi la bwana harusi wapo ndugu wengine, mmoja ataropoka sawa mzee tunatambua mke wa kuoa hayupo, lakini unaonaje kama mke mwenyewe umeshaishi nae miaka mingi na najua umeshamchoka na sisi tunamtaka kumuoa basi tunaomba tukurudishie posa yako ili tuondoke naye.

Babu wa bibi harusi atakubaliana na hoja hii ya kurejeshewa posa yake na atasema nilipeni haraka sana, mmeshanichosha na maneno yenu kwanza nina wake wengine wengi wazuri kuliko huyu.

Babu wa bibi harusi atapokea mitungi ya pombe na kabla ya kunywa pombe hiyo ya mtungi mmoja watakabidhiwa kikundi cha burudani kilichokuwa kinatumbuiza Kishaija Nyabaki. Babu atawaambia wale wanaotaka kuoa kwa kuwasema kuwa nyinyi mnadhani nani anashida na hii pombe yenu, haya maneno yatasemwa huku akinywa pombe na tafsri yake kuwa hapo bibi harusi ataolewa na maombi yao yamekubalika.

Utani wa pili huwa katika siku ya ndoa hii ni siku yenyewe ya harusi. Wakiwa nyumbani kwa bwana harusi, bibi harusi pale anapotaka kuingia ndani ya mlango wa nyumba yao mpya, bibi wa bwana harusi atazuia binti huyo kuingia ndani na bibi huyu atatamka ehh mnampeleka wapi? Hapa bibi harusi atakaa kimya. Bibi wa bwana harusi atauliza tena ninakuuliza wewe tena unakwenda wapi? Bibi harusi atakaa kimya tena. Bibi atasema tena, jamani wewe binti mdogo unaenda wapii? Bibi harusi atakaa kimya tu, kama bubu.

Bibi atasema sawa nitakufundisha adabu, unaenda wapi? Hapa ni kwako? Si unatambua kuwa hapa ni kwangu? Hapa Bwana harusi uzalendo utamshinda atatoa zawadi na mara nyingi huwa ni fedha na kumkabidhi bibi yake na bibi huyu ndipo atakapowaruhusu bwana na bibi harusi kuingia ndani ya nyumba ili waweze kuikamilisha hiyo ndoa yao.Hii shuguli yote inaitwa Okwala Ekitabo

Hapa bibi huyu uwaonesha kitanda cha kulala maharusi hawa.Sasa ya huko chumbani ni ya wawili kama harusi imejibu au la. Huko mie mwandishi simo na wahaya pia hawamo. Lakini nikupe umbea kidogo mara zote bibi harusi lazima awe bikira wakati anafunga ndoa ndiyo maana uwepo wa mabibi hao wakati wote una maana kubwa sana kwa kabila hilo. Jiulize maswali mawili huyu bibi ambaye anaonekana ana wivu kwa mjukuu wake uwepo wake una kazi gani? Kwanini anawakaribisha katika chumba chenye kitanda ambacho kwa hakika kilitandikwa na bibi huyu mwenye wivu. Lakini haya nitakusimulia na utayapata katika simulizi zijazo, leo nasimulia tuu juu ya utani.

Wahaya pia wanautani katika msiba ambapo wao huita kusilibya, mathalani mara baada ya kufariki babu/bibi ambaye huwa na wajukuu na vitukuu kadhaa babu/bibi huyo kwa mfano ana miaka 90. Hapa watu hukusanyika katika msiba huo, ndugu na majirani wote katika eneo hilo lililofiwa. Wajukuu na vitukuu wanakusanyika mbele ya mjukuu mkubwa huku wakiwa na ngoma yao.

Hapo watajenga kibanda kidogo cha matope huku wakianza kuimba, kupinga na kucheza ngoma hiyo kama kuna sherehe. Huku wakisema maneno ya kukera kwa marehemu babu. Wataisimanga maiti kwa kusema kuwa kwaheri umeondoka, sisi tunakwenda kuishi na mkeo. Kama unampenda sana amka ukae nae.Wajukuu wa kiume watasema leo tunaenda kulala nae.Maneno hayo dhihaka yanaambatana na kuchezwa kwa ngoma na kunywa kwa pombe.Wakati vituko hivyo vikiendelea na waombolezaji wengine wakiendelea na maombolezo.

Vituko hivyo vinaendelea hadi siku ya kuzika, basi wakati jeneza lipo nje, wajukuu na vitukuu hawa wanaweza kuja wakachukua jeneza hilo wakilibeba huku wakiimba nyimbo zao mwisho wataruhusu maziko kufanyika baada ya kupewa pesa huku muda mwingine wakiwa na fujo zaidi pesa inaweza kukataliwa. Lakini baadaye wataruhusu mazishi kufanyika. Wakishazika wataendelea kuimba nyimbo na kupinga ngoma kutoka katika kibanda chao kidogo walichojenga huku wakikimbia hadi katika kaburi wakila na kunywa pombe.

Kumbuka kuwa watani huwa hawapigwi na ukimpiga mtani ndugu yangu mtazika wenyewe. Kwa hiyo kama umetaniwa umekasilika kuwa mpole, subiri wenzako wafiwe ukalipize. Basi kwa leo hapa naweka kalamu yangu chini. Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


No comments:

Post a Comment