Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE), Prof. Catherine Msuya akizungumza na washiriki waliohudhuria mkutano huo.
Na Mbaraka Kambona, Dodoma
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema huduma za ugani ni kiungo muhimu katika kuwasaidia Watafiti, Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kufanya uzalishaji wenye tija.
Ulega aliyasema hayo wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) unaoendelea kufanyika jijini Dodoma kuanzia Disemba 1-2, 2021.
"Ni muhimu kwenu Maafisa Ugani kujenga ushirikiano na Wakulima, Wafugaji, na Wavuvi ambao utalenga kuwapa taarifa sahihi, kutumia huduma za ugani kama nyenzo ya kusambaza teknolojia, kuelimisha, kutoa ushauri wa kitaalamu na kupata mrejesho wa matumizi ya teknolojia," alisema Ulega.
Alisema katika juhudi za kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa Maafisa Ugani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) imeandaa mfumo wa kielektroniki unaofahamika 'Huduma za Ugani Kiganjani' kwa ajili ya kuratibu utoaji wa huduma za Ugani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
"Kwa kutumia mfumo huu, changamoto ya uhaba wa Maafisa Ugani itapungua lakini pia ufanisi wa utoaji huduma za ugani utaongezeka," alifafanua.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia taasisi zake za Utafiti imeendelea kuibua teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza na kuboresha uzalishaji wa tija na wa kibiashara katika mazao ya Kilimo, Mifugo na uvuvi.
"Iwapo teknolojia hizi zitatumiwa kikamilifu zitaongeza uzalishaji na tija, hivyo kuna umuhimu Maafisa Ugani kutoa zaidi elimu, Mafunzo na hamasa kwa wananchi na wadau wote ili kuongeza matumizi ya teknolojia hizi," alisisitiza.
Aidha, alisema kuwa katika kuhakikisha Maafisa Ugani wanawafikia wafugaji na kutoa ushauri kwa ufanisi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Sekta ya mifugo imenunua pikipiki 300 na Sekta ya Uvuvi ipo katika mchakato wa kununua pikipiki 10.
Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania ( TSAEE), Prof. Catherine Msuya alisema kuwa pamoja na mipango mizuri waliyonayo ya kuendeleza chama hicho bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha jambo ambalo linafanya Chama kushindwa kuendesha shuguli zake kama inavyotakiwa.
Aliongeza kwa kusema kuwa miongoni mwa malengo makuu ya Chama hicho ni kuwa na jukwaa la kubadilishana uzoefu, kuboresha sera zinazoongoza utendaji wa ugani, na kufuatilia matatizo yanayokabili fani ya ugani kwa lengo la kudumisha mawasiliano katika kutatua matatizo hayo kwa maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Afisa Ugani kutoka Wilaya ya Chamwino, jijini Dodoma, Devota Utaselwa alisema kuwa mkutano huo utawawezesha kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatawasaidia kuboresha utendaji kazi wao na pia watapeleka elimu hiyo kwa wenzao ambao hawajafika katika mkutano huo na Wananchi wanaowahudumia ili waweze kuzalisha kwa tija.
No comments:
Post a Comment