Akizungumza jana Jijini Arusha kwenye Mkutano wa Kisekta wa Baraza la Mawaziri wa Utalii na Wanyamapori wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya Mtandao, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro aliwaeleza Mawaziri hao kuwa Tanzania ipo tayari kuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Waziri Ndumbaro alilitoa ombi hilo mara baada ya Burundi aliyetakiwa kuwa mwenyeji wa Maonesho kutokuwa tayari kuyafanya kwa mwaka huu na hivyo kuahidi kuwa atakuwa tayari mwakani, hali hiyo ikailazimu Tanzania kuomba na kisha kukubaliwa kuwa Mwenyeji wa Maonesho hayo.
Alisema lengo la Maonesho hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ni kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi hizo.
Alisema makubaliano hayo ya kuanzisha maonesho hayo ni hatua mahsusi kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kujitangaza baadala ya kutegemea makampuni makubwa ya utalii kutoka nje kutangaza vivutio hivyo kwa namna makampuni hayo yanavyotaka yenyewe.
Akizungumza katika mkutano huo, Dkt.Ndumbaro amewaelezea Mawaziri hao kuwa maonesho hayo ya Utalii nchini Tanzania ni hatua muhimu ya kuwatia nguvu sekta binafsi ya kuona namna ya kujipanga upya kurudi katika biashara ya utalii kutokana na ugonjwa wa UVIKO kuitikisa vibaya sekta hiyo.
Alisema athari za ugonjwa wa UVIKO 19 umedumaza Makampuni binafsi na hivyo kupelekea kupunguza idadi ya wafanyakazi wa sekta na hivyo kuongeza tatizo kubwa ajira nchini
"Kwa vile Burundi imeonesha kutokuwa tayari, Sisi Tanzania tupo tayari kufanya Maonesho hayo kwa mwaka huu ikiwa lengo letu kutuma ujumbe kwa mataifa makubwa kuwa tupo tayari kuwapokea na kuwahudumia watalii" alisisitiza Dkt.Ndumbaro
Katika hatua nyingine Tanzania imeendelea kushikilia msimamo wake wa kuomba muda zaidi wa kujiandaa kujiunga kwenye Visa ya pamoja ya Watalii.
Akifafanua katika mkutano huo, Waziri Dkt.Ndumbaro aliwaeleza Wajumbe hao kuwa suala viza ya pamoja ya utalii kwa Tanzania ni suala nyeti na linahusisha mamlaka zaidi ya moja katika kufanya maamuzi hivyo inaomba ipewe muda zaidi kwa ajili ya kuweza kufikia maafikiano na mamlaka zingine hususana mamlaka ya uhamiaji na usalama.
Alisema suala la visa ya pamoja ya utalii linahitaji makubaliano ya ndani kwanza kabla Tanzania haijaamua kujiunga nayo suala ambalo mjadala wake wa kuitaka Tanzani kujiunga liliungwa mkono kwa nguvu sana na Mawaziri wa kutoka nchini Kenya pamoja na Uganda.
Licha ya mjadala huo kuchagizwa na Mawaziri hao, Dkt. Ndumbaro alisema suala la viza ya pamoja ni muhimu kibiashara lakini linagusa usalama wa nchi na hivyo aliwashauri Mawaziri hao liache liamuriwe na mamlaka zingine ikizingatiwa kuna Tanzania bara na Tanzania Visiwani.
Katika Mkutano huo ulihudhuriwa na Mawaziri wote wenye dhamana ya utalii na wanyampori kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kutoka Tanzania, Kenya Uganda, Sudani pamoja na Rwanda.
No comments:
Post a Comment