RAIS DK. HUSSEIN MWINYI AWAPIGA 'MKWALA' WAKANDARASI MRADI WA MAJI EXIM BANK - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 9 July 2021

RAIS DK. HUSSEIN MWINYI AWAPIGA 'MKWALA' WAKANDARASI MRADI WA MAJI EXIM BANK

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Na Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Wakandarasi wa Mradi wa Maji wa Exim Bank kuelewa kuwa mradi huo unapaswa kukamilika kwa wakati kama ulivyopangwa.

Dk. Mwinyi ametoa muongozo huo leo wakati alipotembelea mradi wa Maji wa Exim Bank ulioko Dole, Wilaya ya Magharibi A, ikiwa mwanzo wa ziara yake ya kukaguwa shughuli za maendeleo na kusikiliza changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi. Amesema pamoja na mradi huo kuchelewa kuanza kwa wakati, umekuwa na kasoro na urasimu katika utekelezaji wake.

Alisema mradi huo mkubwa unaogharimu zaidi ya Dolaza Kimarekani Millioni 92.18 ni wa miezi 18, hivyo ni lazima ukamilike kwa wakati na kukabidhiwa Serikalini pale muda uliopangwa utakapofika. Alisema sababu zote zilizotolewa kukwamisha hatua ya kuanza mradi huo, ni mambo yalio ndani ya uwezo wa watendaji wa Mamlaka inayohusika.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitembelea Visima Vibovu eneo la Welezo pamoja na Visima vya maji vilivyoko Bumbwisudi na kusema huduma za maji safi na salama zitaweza kupatikana ndani ya kipindi kifupi, kijacho kupitia njia ya muda mfupi na muda mrefu.

Alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) itachukua hatua za kuweka Pump mpya za kusukuma maji katika maeneo ambayo pump zake zimeharibika pamoja na kutengenza matangi ili maji yaweze kupatikana.

Ameutaka Uongozi wa Mamlaka hiyo kuwajibika na kuwa karibu na wananchi ili uweze kutatua changamoto mbali mbali ziliopo za ukosefu wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.

Naye, Mwakilishi wa Jimbo la Bububu Mudrik Ramadhan Soraga, alisema mradi wa Axim Bank ni mwarobaini katika utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama, sio tu kwa Jimbo la Bububu, bali kwa Wilaya A, B pamoja na Wilaya Kati.

Waziri Soraga alibainisha umuhimu wa Serikali kuondokana na utaratibu wa kuwa na miradi mingi na kuchimba kisima kimoja kimoja na badala yake kuwa na mradi mmoja utakaohusisha uchimbaji wa visima vingi.

Aidha, Mkurugenzi Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Dk. Salha Mohamed Kassim alisema mradi wa maji wa Axim Bank unaolenga kuhuishaji na kuimarisha huduma za upatikanaji wa maji, unagharimu zaidi ya Dola za Kimarekan Milioni 92.18, ikiwa ni fedha za Mkopo kutoka Exim Bank ya India.

Alisema mradi huo utahusisha uchimbaji wa visima 64 pamoja na matangi 14 ya Ardhini pamoja na juu ya Mnara. Dk. Salha alizitaja sababu mbali mbali zilizofanya mradi huo ushindwe kutekelezwa kwa wakati uliopangwa, ikiwemo ile ya ufunguzi wa huduma maalum za malipo, kuchelewa kwa kibali cha ujenzi wa matangi ya maji, misamaha ya kodi na kusema rasilimali ya mchanga utakaotumika kwa ajili ya ujenzi wa matangi hayo itaagizwa kutoka Tanzania Bara.

Mkurugenzi huyo aliahidi kusimamia kikamilifu na kwa ufanisi mkubwa mradi huo. Katika hatua nyengine, kwa nyakati tofauti Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kutembelea barabara za Masingini, Mwachealale na Barabara ya Kibondeni, na kuwahakikishia wananachi hao kuwa barabara hizo zitajengwa kwa kiwango cha Lami, kupitia Bajeti ya Serikali ya 2021/2022.

Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, alisema kukamilika ujenzi wa barabara hizo, mbali na kurahisisha usafiri lakini pia zitachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo husika.

Aidha, Dk. Mwinyi alisikiliza changamoto mbali mbali za wananchi katika maeneo mbali mbali aliyoyatembelea na kuzitolea ufafanuzi. Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Bububu huko Dole, Rais Dk. Mwinyi aliwataka wananchi hao kumpa muda ili aweze kufahamu kile kilichoamuliwa na Mahakama , ili hatimae Serikali iangalie `namna ya kushughulikia mgogoro mkubwa wa Ardhi uliopo kati ya wananchi na Bi Shafika.

Akachukua fursa hiyo kukipongeza Kikosi cha KMKM Masingini kwa kazi nzuri wanazofanya pamoja na kukipatia Gari la Wagonjwa ili liweze kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji kusafirishwa kufuata huduma katika Hospitali nyengine.

Aidha, aliagiza Soko la zamani liliopo Bububu lirudishwe mikononi mwa wananchi, huku akiwataka polisi wabakie na jukumu la kulinda usalama wa wananchi na mali zao. Kuhusiana na katazo la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kizimbani dhidi ya wananchi wanaoishi karibu na eneo hilo la kusitisha shughuli zote za ujenzi katika nyumba zao, Dk. Mwinyi alisema suala hilo litapatiwa ufumbuzi hivi karibuni baada ya kujua ukubwa wa tatizo lenyewe.

Aidha, akaitaka ZECO kujipanga vizuri na kuhakikisha wananchi wanaohitaji huduma za kuungiwa umeme katika nyumba zao, wanapata huduma hiyo kwa gharama nafuu, pamoja na kuwaondolea mzigo wa ununuzi wa nguzo, kwa kigezo kuwa hawana uwezo wa kununua nyenzo hiyo. Dk.Mwinyi akabainisha kuwa kuanzia sasa hivi vijana wote wanaofanyakazi za kujitolewa katika taasisi za serikali, watapewa kipaumbele katika suala la upatikanaji wa ajira pale zinapotokea.

Nao, baadhi ya wananchi walimuelekza Rais Dk. Mwinyi ya kuwepo changamoto mbali mbali zinazowakwaza, ikiwemo ukosefu wa huduma za maji safi, ubovu wa barabara, migogoro ya ardhi, mahitaji ya Vituo vya Polisi,ukosefu wa ajira, ahadi za Viongpozi na nyenginezo. Katika ziara hiyo, pamoja na mambo mengine Dk. Mwinyi alipata fursa ya kutembelea Skuli ya Abdalla Sheria Tomondo, Kukagua mradi wa Maji wa Exim Bank Kwarara Kidutani, Barabara ya Kibondeni, Mradi wa Maji wa Exim Bank Dimani oamoja na Mardi wa Maji wa Exim bank Maungani.

No comments:

Post a Comment