Na Josephine Majura, Arusha
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, ametoa wito kwa Wahariri nchini kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili waweze kutumia fursa zilizopo ili kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Alitoa wito huo wakati akifungua semina ya siku 2 kwa Wahariri kutoka Vyombo mbalimbali vya Habari nchini iliyofanyika jijini Arusha, ambapo amewataka Wahariri hao kuzisema fursa zilizopo ili kutoa nafasi kwa wawekezaji kuweza kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kwa njia ya ubia ili kuboresha huduma za jamii. ’’Serikali imeandaa programu ya PPP nchini ili kuwezesha Sekta Binafsi kushirikiana na Serikali kuhakikisha inatekeleza miradi ya maendeleo iliyopo katika Sekta mbalimbali," alisema Tutuba. Alisema Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea kushirikiana na vyombo mbalimbali vya Habari ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu nzuri kuhusu masuala ya ubia kwa kuwa wakiwa na uelewa sahihi wengi watavutiwa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali nchini na kufanya uchumi wa nchi kupanda. Bw. Tutuba, amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini ili kuvutia wawekezaji kwa kuwa miradi mingi inahitaji wawezekaji kama vile miradi ya barabara, reli pamoja na madaraja. Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Dkt. John Mboya, alisema kuwa utaratibu wa ubia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ni njia muhimu sana ya vyanzo mbadala vya kugharamia miradi ya maendeleo kwa kuwa mapato ya Serikali pekee hayatoshi kugharamia miradi ya maendeleo. “Serikali imetunga Sera ya PPP ya Mwaka 2009, Sheria ya PPP Sura 103 na Kanuni za PPP za Mwaka 2020 ili kuweka mazingira wezeshi ya kuishirikisha Sekta Binafsi kwa utaratibu huo wa PPP”, alisisitiza Dkt. Mboya. Aliongeza kuwa hadi mwezi Mei, 2021 jumla ya miradi 41 kutoka Sekta ya Mawasiliano, Ujenzi, Afya, Elimu, Biashara na Maji ipo katika hatua mbalimbali za maandalizi, ikiwa na makadirio ya thamani ya sh. Trilioni 3.042. Naye Mwenyekiti wa Mkutano huo wa Wahariri Bw. Ben Mwangónda aliipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuendelea kufanya semina mbalimbali kuhusu majukumu ya Wizara kwa kuwa semina hizo zimewajengea uwezo kwenye taaluma zao katika kutoa taarifa kwa ufanisi kwa wananchi kama ilivyokusudiwa. Aliahidi kuwa kwa niaba ya Wahariri walioshiriki semina hiyo atahakikisha vyombo vya Habari vinatoa elimu mbalimbali kuhusu masuala ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuwawezesha wawekezaji kuongezeka nchini kwa kuwa elimu inahitajika kwa jamii. Semina ya Wahariri inafanyika kwa 2 mbili mkoani Arusha ambapo imejumuisha jumla ya Wahariri 38 kutoka vyombo mbalimbali vya Habari nchini ikiwa ni mwendelezo wa Semina zinazoratibiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ili kuwajengea uwezo wahariri na wanahabari kwa ujumla kuhusu majukumu ya Wizara hiyo. |
No comments:
Post a Comment