KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Malongo, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kuhakikisha unaboresha huduma zake na kuongeza ufanisi kwa watumishi wake ili kuvutia wateja wao ambao wamekuwa wakilalamika kuhusu utoaji wa huduma zao.
Akizungumza katika uzinduzi wa karakana sita zinazohamishika (Mobile Workshop), vifaa stahiki vya kuchunguza ubovu wa magari pamoja na viti 33 vya wenye mahitaji maalum kwa ajili ya kusaidia abiria wanaovuka katika vivuko vyote nchini vinavyosimamiwa na Wakala huo.
Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa licha ya Wakala huo kuwa na Karakana kila Mkoa, lakini bado huduma zinazotolewa ndani ya karakana hizo haziridhishi hali inayopelekea washitiri kuamini kuwa Wakala umebweteka kutokana na kukosekana kwa ushindani wa kibiashara na kuwa ni Taasisi ya Serikali pekee kwenye matengenezo ya magari.
“Nilivyoingia Wizarani mwezi wa tatu, niliamua kufanya utafiti kwa baadhi ya Taasisi za Serikali kuhusu utendaji wa TEMESA, nilifanya hivyo kwa sababu nilikuwa mlalamikaji kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala huu, na matokeo niliyopata kutokana na utafiti wangu ni kuwa, asilimia 75 ya niliowahoji walisema kuwa TEMESA wamebweteka na pia wafanyakazi wao kutokuendana na mabadiliko ya teknolojia”, amesema Mhandisi Malongo.
Ameongeza kuwa utafiti ulibaini kuwa Wakala huo umetawaliwa na ukiritimba, ukosefu wa uweledi kwenye kazi na ubadhirifu wa vipuri ambapo baadhi ya vifaa vinavyofungwa katika magari si halisi na huharibika muda mfupi mara tu baada ya kupatiwa huduma.
Aidha, ameusisitiza Wakala huo kuhakikisha wanaboresha mkakati wao wa kibiashara na kuboresha usimamizi wa kifedha ambao utalenga kutoa huduma nzuri kwa wateja wao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa Wakala huo, Profesa Idrissa Mshoro, ameiomba Serikali kupitia Wakala huo kuendelea kuajiri mafundi wa kutosha ili kuongeza idadi ya mafundi na kuwapatia ujuzi utakaoendana na mabadiliko ya teknolojia ambayo yatawasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Maselle, amesema kuwa, ununuzi wa wa karakana zinazohamishika umelenga kusogeza huduma kwa wateja waliombali na karakana za mikoa na pia kutoa huduma ya matengenezo ya dharura yanayotokea maeneo yasiyo na karakana hasa magari na mitambo yanapokuwa safarini au kazini nje ya ofisi.
Ameongeza kuwa viti vya wenye mahitaji maalum vitakuwa msaada kwa abiria wenye ulemavu ambapo awali huduma hii ilikuwa haitolewi kwenye vivuko vya Serikali na kusababisha usumbufu kwa abiria wenye mahitaji maalum.
Kuhusu vifaa vya kuchunguza ubovu wa hitilafu za magari na mitambo, Mhandisi Maselle, amesema kuwa Wakala umepanga kupeleka vifaa hivyo katika kila kituo na kufafanua kuwa vifaa hivyo vitasaidia kubaini tatizo kwa usahihi na kwa muda mfupi, kutaboresha huduma na kupunguza muda wa matengenezo ya magari na mitambo pamoja na kupunguza malalamiko ya wateja kufungiwa vipuri visivyo halisi.
Zaidi ya shilingi Milioni 765 zimetumika katika ununuzi wa karakana sita zinazohamishika ambazo zitagawiwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya,Tabora na Dodoma, ununuzi wa vifaa 30 vya kuchunguza ubovu na hitilafu za magari na mitambo pamoja na viti 33 vya wenye mahitaji maalum.
No comments:
Post a Comment