Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini wa Mpango wa Kurasimisha Risilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Anthony Temu akimuelekeza jambo kwenye simu janja mmoja wa vijana wa jamii ya wafugaji, Mussa Letema wakati wa zoezi la kukusanya taarifa za dodoso kupitia mfumo wa Kobo wakati wa mafunzo ya kuwawezesha kiuchumi watu wa jamii ya wafugaji kwa kutumia hatimiliki za kimila za kumiliki ardhi kuweka kama dhamana kukopa fedha benki za kusaidia kuboresha mfumo wa ufugaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi mingine ili kuinua kipato chao.
Na Mwandishi Wetu- Mbarali
WAFUGAJI 58 wa jamii ya Wamasai wilayani Mbarali mkoani Mbeya wamenufaika na mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kujikwamua kiuchumi yaliyofanyika katika kijiji cha Mogelo, wilayani humo mwishoni mwa wiki ili kuwawezesha kuendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayolenga kuendelea kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi wote.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) yamejikita katika kuwezesha jamii hiyo ya wafugaji kutumia hatimiliki za kimila za kumiliki ardhi kukopa fedha katika taasisi za fedha kama benki ili kukuza shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Awali akieleza kuhusu mafunzo hayo, Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini kutoka MKURABITA, Bw. Antony Temu alisisitiza kuwa” Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwawezesha wanufaika wote wa mafunzo kutumia hatimilki zao kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo inayotolewa na taasisi za fedha ili dhamira ya Serikali kumuwezesha kila mwananchi iweze kutimia kwa wakati.”
Aidha, Bw. Temu alieleza kuwa mada zilizowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na; faida za kujiunga na ushirika, mbinu za ufugaji bora, kanuni za kilimo bora cha mazao mbalimbali, utunzaji bora wa kumbukumbu na usimamizi bora wa rasilimali zinazoizunguka jamii hiyo.
Wawezeshaji katika mafunzo hayo walikuwa wataalamu wa kilimo, ushirika, ardhi, na ufugaji nyuki kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Mbarali na wataalamu wengine ni kutoka katika taasisi za fedha ikiwemo Benki ya CRDB na NMB.
MKURABITA imekuwa ikiowajengea uwezo wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kuendesha mafunzo ya namna bora ya kutumia hatimiliki za kimila za kumiliki ardhi kijiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii ili kuendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita baada ya kurasimisha maeneo yao na kupatiwa hatimiliki hizo.

No comments:
Post a Comment