MAJALIWA AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKI ZOEZI LA SENSA2022 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 22 May 2021

MAJALIWA AWATAKA WANANCHI KUSHIRIKI ZOEZI LA SENSA2022

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali Bw. Emmanuel Tutuba, akitoa maelezo ya awali wakati wa tukio la  Uzinduzi wa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022, tukio lililofanyika katika viunga vya Ofisi ya taifa ya Takwimu jijini Dodoma.

Na Farida Ramadhani na Saidina Msagi, Dodoma

WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mwaka 2022 ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo, kupunguza umasikini na kukuza uchumi.

Mhe. Majaliwa ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati akizindua Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kilichoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

“Matokeo ya sensa yataiwezesha Serikali kupata takwimu za msingi zinazotumika kuakisi hali halisi iliyopo na kupanga mipango ya maendeleo kwa kutunga sera pamoja na kupanga mipango, program na kufuatilia utekelezaji wake”, alisema Mhe. Majaliwa.

Alisema ni muhimu wananchi watoe ushirikiano kwa wakusanya takwimu ili kuliwezesha zoezi hilo kuenda vizuri na kuleta matokeo tarajiwa kwa maendeleo ya nchi.

Aidha, aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuanza kutoa elimu ya umuhimu wa sensa kwa wananchi ili kuwaweka tayari kushiriki zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdallah alisema kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, sensa ya watu na makazi ni miongoni mwa sehemu muhimu katika Muungano wa Tanzania.

Alisema anaamini kuwa sensa ya mwaka 2022 itakuwa ya kipekee kutokana na juhudi za viongozi na wataalamu waliopo ambao wamesha ainisha changamoto zote zilizojitokeza katika sensa zilizopita na kupanga namna bora ya kuzitatua kwa ajili ya kuboresha.

Naye Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), alisema Serikali inawajibu wa kuandaa zoezi la sensa ya watu na makazi ili kupata idadi kamili ya watu na kuweza kupanga maendeleo ili kukuza uchumi.

Alimhakikishia Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kuwa Ofisi za Taifa za Takwimu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zitahakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi mkubwa.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba alisema kuwa Uzinduzi wa Kitabu cha Mkakati wa Usimamizi wa Utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ni alama kuu ya uzinduzi rasmi wa shughuli za maandalizi ya sensa hiyo ambayo majaribio yake yatafanyika Agosti, 2021.

Alitoa rai kwa wadau wa maendeleo na mashirika ya kimataifa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia rasilimali fedha, vifaa na utaalamu kwa muda wote wa maandalizi hadi kuhitimisha zoezi hilo.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Alibina Chuwa alisema sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ni sensa ya sita kufanyika nchini ambapo sensa ya kwanza ilifanyika 1967, ya pili 1978, ya tatu 1988, ya nne 2002 na ya tano 2012.

Alisema Sensa hiyo itakuwa ya kipekee kwa kuwa itatumia teknolojia ya hali ya juu ili kupata taarifa kuanzia kwenye ngazi ya vitongoji, vijiji na ngazi ya mitaa na mijini wakikusanya taarifa sahihi za idadi ya watu, umri, elimu na upatikanaji wa huduma za kijamii kama maji, umeme na afya.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) hapa nchini, Bi. Jacqueline Mahon alisema shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Serikali katika kufanikisha utelezaji wa sensa hiyo kwa kuhakikisha kuwa kila mtu anahesabiwa na takwimu sahihi zinapatikana kwa urahisi na kukidhi mahitaji ya watumiaji kwa viwango vya kimataifa.

Alisema kukamilika kwa Sensa ya watu na makazi kutaboresha na kuwezesha kuwa na uhakika wakati wa kupanga mipango ya maendeleo ya kitaifa, kupima matokeo na kufuatilia uwajibikaji katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa.

No comments:

Post a Comment