Wakaguzi wa TBS wakiendelea na ukaguzi pamoja na kutoa elimu kuhusu ubora na usalama wa chakula na vipodozi kwa wauzaji wa bidhaa hizo katika Manispaa ya Iringa.
Wakaguzi wa TBS wakiendelea na ukaguzi pamoja na kutoa elimu kuhusu ubora na usalama wa chakula na vipodozi kwa wauzaji wa bidhaa hizo katika Manispaa ya Iringa.
WAKAGUZI wa TBS kutoka Kanda za Nyanda za Juu Kusini wamewataka wamiliki wa maduka ya chakula na vipodozi kusajili na kuuhisha vibali vya majengo ya muhifadhia na kuuzia bidhaa hizo, lengo likiwa ni kujihakikishia kuwa wakati wote wanauza bidhaa bora na salama kwa watumiaji.
Mkaguzi wa TBS Ernest Simon katika ukaguzi huo amewaelimisha wauzaji wa bidhaa za chakula na vipodozi kuhakikisha kuwa wanaponunua bidhaa hizo kuhakikisha kuwa zimethibitishwa ubora wake na TBS kama zimezalishwa hapa nchini pamoja na kuangalia ukomo wa matumizi wa bidhaa hizo.
Kwa upande wa bidhaa za vipodozi Bw. Simon alisema wauzaji wanatakiwa kuhakikisha kuwa wakati wote hawauzi vipodozi vyenye viambata sumu ambavyo ni hatari kwa usalama wa afya za watumiaji na kuongeza kuwa Shirika halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa muuzaji atakayekiuka utaratibu.
"TBS ilishawatumia wadau wote wa vipodozi orodha ya vipodozi visivyoruhusiwa kuuzwa nchini na pia orodha hiyo inapatikana kwenye tovuti ya Shirika, ni muhimu kila mdau kuwa na orodha hiyo ili kuepuka usumbufu wa aina yoyote," alifafanua Bw. Simon.
Wakati huo huo Mkaguzi Mwesigwa Kajumlo amewataka wauzaji wa bidhaa za vipodozi na chakula kuzingatia maelekezo wanayowapatia wakati ukaguzi, ili wanaporudi kwa mara nyingine wawe wameshayafanyia kazi, kwani baadhi yao wamekuwa wakizembea na kuwalazimu wakaguzi kuwaelekeza upya jambo lilelile.
Bw. Mwesigwa alisema itafika kipindi Shirika halitawavumilia wafanyabiashara wanaokaidi maagizo ya Serikali, hivyo ni vyema wakayafanyia kazi maelekezo yanayotolewa na wakaguzi kwani lengo ni kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopo sokoni ni bora na salama kwa watumiaji.
No comments:
Post a Comment