Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) tayari limerejesha gharama za vifurushi vya zamani vya Intaneti, SMS na Dakika, ikiwa ni kutoa fursa kwa wateja na wananchi kuendelea kufurahia huduma za mawasiliano vizuri kama ilivyokuwa awali.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Bw. Leonard Laibu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisi Kuu ya shirika hilo, jijini Dar es Salaam.
Alisema, baada ya maoni mengi kutoka kwa Wananchi, April 02,2021 Serikali ilisitisha gharama mpya za vifurushi na kuagiza watoa huduma za mawasiliano kurejesha vifurushi kama ilivyokuwa awali.
“Katika kutii agizo hilo, Shirika la Mawasiliano Tanzania siku iliyofuata ya April 03, 2021 ilianza na kukamilisha mchakato wa kurejesha gharama za vifurushi vya zamani. Hivyo, kuanzia tarehe hiyo ya Aprili 03,2021 vifurushi vyetu vilikuwa tayari vimeisharejea kama ilivyokuwa awali na kutii agizo la Serikali,” alisema Bw. Laibu.
Aidha ameongeza kuwa kurejea kwa vifurushi vya zamani kumetoa fursa kwa wateja na wananchi kuendelea na kutumia huduma za mawasiliano vema.
“...Tunapenda kuufahamisha Umma wa Watanzania kuwa Shirika linaendelea kuwajali Watanzania na wateja wake kwa ujumla kwa kuwapa huduma bora za mawasiliano ili kukidhi mahitaji yao. Tunapenda kuwataarifu RASMI kuwa vifurushi vyetu vya zamani vyenye gharama nafuu vimesharejea kama kawaida, hivyo tunawaalika watanzania waendelee kufurahia huduma zetu. Wateja wetu wanaweza kupata huduma za vifurushi vyetu kwa kupiga *148*30# au kupitia huduma zetu za kifedha ya T-PESA *150*71#. Alisisitiza Bw. Leonard Laibu.
Afisa Mwandamizi Kitengo cha Biashara, Bw. John Yahya (katikati) akifafanua jambo katika mkutano huo. |
Aliongeza kuwa TTCL inawakaribisha Watanzania ambao hawajarudi Nyumbani, basi watembelee mawakala wao ambao wamesambaa maeneo mbalimbali nchini au kutembelea Vituo vya Huduma kwa Wateja ili waweze kusajili laini zao, sambamba na kupata huduma nyingine za mawasiliano.
Amesema TTCL inawahakikishia kuendelea kutoa huduma za mawasiliano kwa weledi na ubunifu ili kukidhi mahitaji ya wateja wetu na Watanzania kwa ujumla. Shirika la Mawasiliano Tanzania linawatakia Waislamu wote Mfungo Mwema wa Ramadhani.
No comments:
Post a Comment