SONGWE KUJIFUNZA USAFI WA MAZINGIRA NJOMBE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 20 April 2021

SONGWE KUJIFUNZA USAFI WA MAZINGIRA NJOMBE

Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt Seif Shekalaghe na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Katarina Tengia Revocati wakijadili jambo ikiwa ni sehemu ya ziara ya Viongozi wa Mkoa wa Songwe kujifunza Utekelezaji wa kampeni ya Usafi wa Mazingira Mkoani Njombe.

MKUU wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela leo ameongoza viongozi na wataalamu wa Afya Mkoa wa Songwe kufanya ziara ya kujifunza utekelezaji wa kampenzi ya usafi wa mazingira kwa Mkoa wa Njombe ambao unafanya vizuri kwa sasa kitaifa.

Brig. Jen. Mwangela amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza ili kuongeza ujuzi na maarifa yatayowezesha Mkoa wa Songwe kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa kampeni hiyo kwakuwa sasa bado mkoa huo haufanyi vizuri.

“Nawapongeza sana Mkoa wa Njombe kwa kufanikisha kufanya vizuri katika usafi wa mazingira, sisi tupo tayari kujifunza ndio mana nimekuja na timu kubwa ya viongozi wote, tunataka kuijua siri ya mafanikio yenu.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.

 Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt Seif Shekalaghe amesema ziara hii itasaidia pia kujitathimini endapo suala la usafi wa mazingira ni ajenda inayoshikiliwa na viongozi wa ngazi zote kuanzia ngazi ya vijiji hadi wilaya kwani tangu tumepata uhuru zaidi ya miaka hamsini suala la usafi wa mazingira bado ni tatizo.

Dkt Shekalaghe amesema kila kiongozi anapaswa kujiuliza endapo anaitendea haki nafasi yake na kama kungekuwa na ushirikiano na kujitoa kwa viongozi wa ngazi zote tatizo hilo lingekua limeisha.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Hamad Nyembea amesema Mkoa wa Songwe haufanyi vizuri katika usafi wa mazingira licha ya kwamba hautofatiani na mikoa mingine kwa maana ya wataalamu wa afya na fedha zinazotolewa na serikali.

Dkt Nyembea amesema ziara hiyo itasaidia wataalamu wa Afya kujua na kushuhudia kwa kujionea wenyewe mbinu walizotumia wenzao wa Mkoa wa Njombe wakafanikiwa katika usafi wa mazingira.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Marwa Mwita Rubirya amesema mkoa huo ulianza kutekeleza kampeni ya usafi wa mazingira mwaka 2012 wakati Mkoa huo una anzishwa na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama UNICEF wamefanikiwa kufanya vizuri kitaifa na kupata zawadi ya magari, pikipiki na fedha.

Rubirya amesema katika kutekeleza kampeni hiyo wamehakikisha wananchi na taasisi zote wanajenga vyoo na kuvitumia, jamii ilihamasishwa kuweka mazingira safi na kuzingatia kanuni bora za afya na kubadili tabia ya kuishi kwa mazoea mabaya ya uchafu.

Amesema kutokana na jitihada walizoweka hadi kufikia Disemba 2020 asilimia  77 ya kaya zote Mkoani Njombe zina vyoo bora, huku asilimia 68 ya kaya zina vyoo na vifaa vya kunawia, asilimia 42 ya shule za msingi na sekondari zina vyoo bora huku vituo vyote vya kutolea huduma za afya vikiwa na vyoo bora.

No comments:

Post a Comment