SHERIA YA USALAMA BARABARANI KWA VYOMBO VISIVYO VYA MOTO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 10 April 2021

SHERIA YA USALAMA BARABARANI KWA VYOMBO VISIVYO VYA MOTO

 


SHERIA YA USALAMA BARABARANI KWA VYOMBO VISIVYO VYA MOTO

LEO tunazungumzia sheria ya usalama barabarani kuhusu vyombo visivyo vya moto kama vile Baiskeli, Mikokoteni ya kukokotwa na wanyama, na Matumizi ya Wanyama barabarani. Tutaona ni kwa jinsi gani sheria inadhibiti matumizi ya vyombo hivi. 


1. UENDESHAJI WA BAISKELI

Kwa mujibu wa  kifungu cha 101 cha RTA ni marufuku: 

(a) Kupakia abiria zaidi ya mmoja (mishkaki) kwenye baiskeli 

(b) Kumpakia kwenye baiskeli mtu aliye chini ya miaka 7.

(c) Kumpakia mtu kwenye baiskeli mahala pengine zaidi ya kwenye kiti cha abiria au keria(carrier). 

Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 107, ni baiskeli inatakiwa kuendeshwa barabarani huku ikiwa na kengele au kifaa kingine chochote kwaajili ya kuashiria. Na mtu anayeendesha baiskeli kila inapofaa atatakiwa kupiga kengele. Aidha kwa mujibu wa kifungu cha 39C, baiskeli kama ilivyo gari inapaswa kuwa na taa kwaajili ya matumizi nyakati za uoni hafifu barabarani. 

Pia mpanda baiskeli kama alivyo mtumiaji mwingine yeyote wa barabara anatakiwa kuendesha kwa kufuata kanuni na taratibu za usalama barabarani. 

Iwapo atakiuka sheria basi atakuwa ametenda kosa na faini yake barabarani papo kwa papo ni shilingi 20,000. 


2. KUHUSU MIKOKOTENI.

(a) Sheria katika kifungu cha 100 inataka mtu yeyote anayesukuma mkokoteni au kuendesha mkokoteni au kupanda mnyama yeyote(kama vile Farasi au punda) na kumtumia kama usafiri kuzingatia sheria za usalama barabarani na hivyo ataongozwa na vifungu vya RTA. 

(b) Kwa mujibu wa kifungu cha 105 mtu yeyote atakayendesha au kusukuma au kusababisha kuendeshwa au kusukumwa kwa mnyama au gari la kukokotwa na wanyama barabarani kwa uzembe, kupuuzia ama kutojali au kwa spidi ambayo ni hatarishi au kwa namna ambayo ni hatari kwa umma au mali, atakuwa anatenda kosa.

(c) Kwa mujibu wa kifungu cha 106, mtu yeyote anayeendesha au kusukuma mkokoteni au mnyama barabarani huku akiwa amelewa atakuwa anatenda kosa. 


3. MATUMIZI YA WANYAMA.

Ni marufuku kwa mmiliki au msimamizi wa wanyama kutumia wanyama wasioona au wenye uoni hafifu barabarani kwaajili ya kukokota mkokoteni.

Kufikia hapo utakuwa umeongeza maarifa kuhusu sheria inavyosema kwa watumiaji hawa wa barabara. 

MASWALI.

1. Umewahi kuona askari wa usalama barabarani wanakamata baiskeli zisizo na taa, riflekta, au kengele? Kama jibu ni NDIYO, wapi? Kama jibu ni hapana unadhani kwa nini?

2. Umewahi kuona askari wanapima ulevi waendesha baiskeli au wasukuma mikokoteni? Kama NDIYO ni wapi, na kama HAPANA, unadhani kwa nini?

3. Je, umewahi kuona askari wanawakamata wapanda farasi, punda, wasukuma mikokoteni, au waongoza wanyama wanaovuta mikokoteni?  Kama NDIYO ni wapi, na kama HAPANA, unadhani kwa nini? 

Ndo maana, makosa ya barabarani ni mengi sana. 

RSA Tanzania

Usalama Barabarani ni Jukumu Letu Sote

No comments:

Post a Comment